MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUAMUA KUBEBA MIMBA!


MAANDALIZI  kabla ya ujauzito yanasaidia kumwezesha mama kuwa na afya bora wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua na kumwezesha kuzaa mtoto mzuri na mwenye afya. Mambo haya hayaji kwa kujipanga ukishapata mimba bali ni kabla ya kupata mimba. Wanawake wengi mara tu baada ya kuwa wajawazito huanza kupata matatizo mengi ya kiafya, kijamii na kiuchumi.

Wengine hadi husema kuwa mimba hiyo imepatikana kwa bahati mbaya. Hali hii ya bahati mbaya husababisha mwanamke achukue maamuzi ambayo hakuyatarajia ya kuitoa kwa namna yoyote mimba hiyo, hivyo akaanza kupata matatizo yanayoathiri mfumo wake wa uzazi. Kipindi hiki pia utajikuta unaingia katika migogoro kama ni mwanafunzi ndiyo inakuwa mwisho wa kuendelea na masomo yako. Unapofikisha umri wa kuzaa yaani unapovunja ungo tu ni vizuri ukaanza kujiwekea malengo na kudhamiria jambo kubwa unalotaka kulifanya katika maisha yako bila kuingiliana na ujauzito.

MATATIZO WAKATI WA UJAUZITO
Kujipanga kabla ya kuamua kuwa mjamzito kunasaidia kuepuka matatizo mengi. Matatizo kabla ya kuwa mjamzito yanaweza kuathiri hali ya ujauzito na baada ya ujauzito. Matatizo haya ni ya kimahusiano, mahusiano yako na mumeo au mpenzi wako.

Hali hii inaweza kukuathiri kisaikolojia, kiuchumi na hata kiafya. Hakikisha kabla ya kujipanga kuwa mjamzito unaweka sawa mambo ya kimahusiano na hata na ndugu na majirani. Magonjwa ya zinaa na mfumo wa uzazi pia ni matatizo yanayoweza kuathiri uzazi au upatikanaji wa ujauzito, kwa hiyo fanya uchunguzi kama umeathirika na magonjwa ya ngono au Ukimwi kwa faida yako na mtoto utakayemzaa.

Magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la damu ni vizuri yachunguzwe mapema kabla ya kuwa mjamzito maana yanaathari kubwa kwa afya ya mama na mtoto aliye tumboni. Mama anayetarajia kuwa mjamzito aepuke ulevi wa aina yoyote, uvutaji wa sigara na misukosuko kwani vyote vinaweza kuathiri aidha upatikanaji wa mimba au mimba zikatoka au mtoto akazaliwa na matatizo.

Matatizo makubwa ya afya ya mama wakati wa ujauzito huweza kusababisha mama akazalishwa kwa upasuaji ili kuokoa maisha yake na mtoto au akapoteza mtoto au yeye mwenyewe akafariki.

MATATIZO WAKATI WA UJAUZITO
Inashauriwa mama mjamzito aanze kliniki mara moja anapokuwa mjamzito, hii itamsaidia kukabiliana na matatizo mengi yanayojitokeza wakati huu au kumuepusha na matatizo baada
ya kujifungua, upungufu wa damu, kifafa cha mimba, maambukizi ya njia ya mkojo na kutapika sana, ni matatizo makubwa yanayoathiri afya ya mama. Mama mjamzito aliyeathirika na virusi vya Ukimwi akiwahi kuanza kliniki ataendelea vizuri na kuja kuzaa mtoto aliye salama.

MATATIZO BAADA YA KUJIFUNGUA
Kutokana na matatizo ya muda mrefu ya afya ya mama wakati wa ujauzito, inaweza kumsababishia matatizo mengi ya kiafya ya kwake na ya mtoto mara tu akishajifungua. Matatizo haya ni kama vile kutokwa sana na damu, kupata homa, kudhoofika mwili, kuchanganyikiwa na upungufu wa damu mara kwa mara, maziwa kutokutoka na matiti kuuma. Mtoto pia anaweza kuugua na kulazwa hospitali kwa muda mrefu, mtoto anaweza kupata ulemavu wa kudumu, uwe wa viungo au akili.

USHAURI Ni vizuri uwahi kliniki mara tu unapokuwa mjamzito. Unapotaka kuwa mjamzito, basi umuone daktari wako akushauri, ili uwe na afya bora.


from Tujifunze Mapenzi https://ift.tt/2EaehG6
via

No comments:

Powered by Blogger.