VICHEKESHO VYA LEO
Hivi karibuni, babu mmoja mwenye mapengo mkazi wa Dar, aligoma kulipa nauli kisa kikiwa kudhalilishwa na kondakta. Tukio hilo lilianza baada ya mpiga debe kuita abiria huku akiongea maneno ya mzaha yaliyosababisha baadhi ya abiria kuyaamini.
“Wenye mimba watalipa mara mbili, wenye mapengo watakwenda bure,” alisema mpiga debe huyo kwa kujiamini wakati alipokuwa akiwaita abiria kupanda ndani ya daladala.
Pembeni yangu alikuwa amekaa babu mmoja aliyekuwa amekunja uso hata kumsalimia niliogopa.
Baada ya daladala kujaza safari ya kuelekea Mwenge ilianza, kumbe babu aliyeketi jirani yangu alikuwa na mapengo hivyo alikasirika kutokana na maneno ya mpiga debe.
Daladala lilipofika Ubungo Gereji lilisimama na yule babu aliteremka, mara akaanza kuzozana na kondakta aliyekuwa akimdai nauli.
“Nimekwambia silipi, si mmesema wenye mapengo bure na kunidhalilisha sasa silipi,” babu alikuwa mkali wote tukaangua kicheko.
“Siwezi kununua pafyumu mimi!”
KATO alikuwa ndiyo kwanza ametoka kazini, amepitia katika Baa ya Makuti iliyokuwa jirani na kazini kwao.
Pale aliwakuta marafiki zake wakiwa wanaendelea kukata kinywaji kama kawaida. Walikuwa ni Julius na Mangeu.
MANGEU: Mh! Kato leo vipi? Nguo zako umerudia kuvaa tena nini?
KATO: Kwa nini?
MANGEU: Kuna kaharufu fulani nakasikia tangu umekuja hapa.
KATO: Inamaana ninanuka jasho?
MANGEU: Sijui lakini ndiyo hivyo au Julius unasemaje?
JULIUS: Mimi sijasikia chochote.
KATO: (Huku akijichekesha) Vyovyote inavyokuwa, lakini nitapata pafyumu muda si mrefu.
MANGEU: Utanunulia wapi baa?
KATO: Kwanza sitanunua, huwa sinunui pafyumu hata siku moja, subiri muuzaji apite ndiyo utajua!
Muda ukaenda, kama alijua vile; Nusu saa baadaye muuzaji wa pafyumu akapita. Kato akamuita na kuanza kuuliza bei na kuomba kujaribu harufu yake kwenye nguo zake.
Alifanya hivyo kwa zaidi ya pafyumu tatu kisha akamwambia muuzaji, hakuna aliyopenda! Hakumuelewa, alimkunja Kato na kumshinikiza anunue moja kati ya zile alizozijaribu.
Si Mangeu wala Julius waliomsaidia. Msala ukawa upande wake. Ilibidi anunue pafyumu moja ya elfu tano. Ujanja wake wote ukaishia hapo!
Auziwa mzoga wa bata
Kweli uswahili kila kukicha hakuishi vituko, juzi kilitokea kituko kilichowaacha watu midomo wazi.
Jamaa mmoja alikuwa akiendesha gari katika mtaa mmoja na kwa bahati mbaya akamgonga bata bila kujua na kuendelea na safari yake.
Watoto wa mwenye bata walikwenda kumwambia baba yao kuwa bata wao ameuawa baada ya kugongwa na gari la jirani yao.
Yule mzee aliwatuma watoto wake wakamlete yule bata, kwa vile ni Waislam hawali mnyama kibudu bila kuchinjwa kihalali ilibidi wamhoji baba yako.
Watoto: Baba bata wa nini amekwisha kufa?
Baba: Nimesema kamleteni.
Watoto: Tumpeleke wapi wakati ulisema mnyama akifa bila ya kuchinjwa tusimle?
Baba: Mimi na nyinyi nani baba?
Watoto: Wewe.
Baba: Haya kamleteni.
Wototo: Lakini sisi hatumli!
Baba: Sitaki ubishi kamleteni.
Watoto hawakuwa na jinsi walimfuata bata na kumpeleka kwa baba yao.
Yule mzee baada ya kupelekewa bata alimweka kwenye mfuko. Jioni alimbeba na kumpeleka kwa jirani yake, alipofika aligonga mlango.
Jirani: Karibu mzee.
Baba: Asante, mzigo wako huu.
Jamaa alipokea huku akiuliza kuwa ni mzigo gani.
Baba: Fungua utaona.
Jamaa alifungua na kushangaa kukuta bata aliyekufa.
Jirani: Hii nini mzee?
Baba: Nilipe gharama ya bata uliyemgonga na kumuua, ukimla sawa ukimtupa utajua mwenyewe.
Jirani: Shilingi ngapi?
Baba: Elfu ishirini na tano tu.”
Jamaa kwa vile hakutaka shari alitoa kiasi hicho cha fedha.
from Tujifunze Mapenzi https://ift.tt/2RIlnpa
via
No comments: