SIMULIZI FUPI TAMU YA KUSISIMUA :BADO NAMKUMBUKA
Miaka saba iliyopita, alikuwa mrembo haswa, alikuwa kila kitu kwangu, rafiki, ndugu, jirani pia mpenzi.Halikuwa jambo la ajabu nilipotafutwa aliulizwa naye alipokuwa akitafutwa nilitafutwa mie walijua tupo pamoja.Darasani tulikuwa pamoja ingawa alikuwa kidato kimoja nyuma yangu ,uwanjani wote tulicheza mpira wa wavu hata UMISETA haikututenga bali tulikuwa pamoja, mitaani ,kanisani hata siku ya disco tulicheza pamoja.Kwa kifupi tulijiona 'mwili mmoja'.....
Si mwingine bali Alice mwanamke aliyeniingiza kwenye ulimwengu wa kikubwa kama mchezo na nikajikuta nikiufurahia ulimwengu huo, niliowakera walikuwa wengi ingawa kulikuwa na wachache waliofurahia mahusiano yetu na wengine ambao hawakujua wawe upande upi...nakumbuka wimbo wa AT na Marlow "wanimaliza" ulivuma kipindi penzi letu lipo juu.... Maskini Alice wangu, mrembo aliyekuja kujutia kitendo chake cha kunikabidhi pendo lake kwa kitendo kibaya nilichomfanyia bila kunikosea.
Kweli Alice aliyajutia maamuzi yake ya kunipenda,kuniona mwanaume sahihi wa maisha yake kuniona mtu mwenye makosa ambayo alikuwa tayari kuyavumilia.Lakini nilipoondoka na kwenda kidato cha tano kwenye shule moja jijini Mwanza nikajikuta namsahau taratibu, na nikajiona mjinga kuuona uzuri usoni na mwilini mwake.Nikaanza kuzikumbuka kasoro zake, hakuwa mweupe ,hakuwa 'modo' kama wengi niliowaona wazuri shuleni na mitaani, hakungea kiswahili kilichonivutia kama wasichana wengi darasani kwetu.
Ghafla nikamchukia kwa kunifanya nimpende na kunipotezea muda, sikumhurumia kwanza nilizichana picha zake ambazo daima nilikuwa nikizitizama kila nilipotaka kulala nikizibusu, nikachana na kuzichoma kadi zake alizokuwa akinipa tukiwa shuleni ,hata shati zuri la kisasa alilonipa siku ya mahafali yangu wala sikukumbuka, kilio chake siku tulipoagana, nikayaita yale mapenzi 'ya kitoto' nikijiambia "atakuwa kapata mwanaume mwingine bhana, mfupi ka kopo la blueband'' Kwa kifupi nilimwona si kitu lakini....! Baada ya kujifanya nimetambua kasoro za Alice mwanamke aliyejitoa kwangu kwa kila kitu, nikaanza kumtafuta wa kuziba 'mwanya' aliouacha nafsini kwani niliona hukufikia hatua ya kuacha 'pengo'.
Lakini kabla sijaamua kumuacha niliwaza visababu ambavyo ningedai vilikuwa chazo cha kumuacha lakini sikuvipata, nilijaribu kumkera 'aropoke' kwenye simu lakini wapi,nikabuni mchezo wa kumtongoza kwa namba mpya ila wapi mtoto alikuwa kaganda kwangu.Ikafika siku ambayo nilijua iwe isiwe atanaswa na nikamnasa kwa kisa ambacho leo naweza kiita cha kipumbavu eti "aliandika sms kwa herufi kubwa na hakuweka mkato na nukta", nikamuacha.Akili ikatulia kuchagua mrembo shuleni kwetu nilimfikiria Helen binti wa kihabeshi aliyechanganya damu ya Rwanda na Ethiopia lakini kukaa kwake bwenini hakunifurahisha nikamfikiria Violet Mushi dada mkuu lakini tetesi za kuwa alikuwa zaidi ya waumbuaji wa pendapenda nikaachana na fikra hizo hadi nilipomfikiria Harriet jirani yangu mtaani na darasani hapo nikaona poa lakini....!
Harriety msichana mrembo kutokea mkoani Iringa aliyekuwa akiishi na shangazi yake jirani kabisa na nilipokuwa nikiishi na familia ya baba yangu mdogo alikuwa chaguo langu kuziba nafasi ndogo aliyokuwa ameiacha Alice.Kwa kuwa nilikuwa nikisoma naye darasa moja akiwa dawati la pembeni yangu haikuwa kazi ngumu kujenga mazoea 'puuzi' yaliyopelekea ujirani nyumbani na shuleni kabla ya kufanikiwa kuuteka moyo wake 'kimiujiza' kwani tulijikuta tumekula tunda bila hata kuombana ama kuambiana kuwa tulikuwa tukipendana.Kisha tukawa wapenzi.Kipindi hicho Alice hakuacha kunipigia akiomba nimsamehe kama palikuwa ambapo alikosea ,sikutaka kujibu jumbe zake wala kupokea simu yake.Moyoni mwangu nilimweka Harriety hivyo sikutaka kuharibu penzi langu jipya kwa mwanamke ambaye nilijihisi kuwa nimepotea njia kwa kuendelea kushughulika naye, nikabadili namba ya simu kuukwepa 'usumbufu' wake lakini masikini Alice hakukata tamaa alitumia njia zote kupata namba yangu mpya na kunipigia jambo lilimfanya ujute..
Ndiyo alijuta kwani siku ile nilipojua kuwa ameipata namba yangu ya simu kupitia mdogo wangu ambaye alikuwa akisoma kidato cha kwanza na katika shule aliyokuwa akisoma Alice, nikaamua kumwachia simu Harriety ambaye hadi leo hii ninapoandika sijui alimwambia kitu gani kwani niliukuta ujumbe mmoja wa neno "Asante" kutoka kwa Alice.Sijui ni jambo gani ambalo mwanamke yule alimwambia Alice maana hata ninapoandika ujumbe huu nakumbuka sehemu ya barua hii ambayo baada ya miaka miwili ya kukaa nayo bila kuisoma nimeamua kuisoma na kugundua kuwa nilimtenda vibaya sana Alice mwanamke ambaye alinipenda sana na nahisi ananipenda hadi leo huko aliko.
Mpenzi najua unajua jinsi gani nakupenda licha ya maumivu makali uliyoniachia moyoni mwangu lakini naomba ukumbuke kuwa nakupenda na nitakupenda milele japo nina hakika siwezi kuwa wako tena.Si kwa sababu unaye ambaye anakupa kiburi na kukufanya uhisi kuwa hunihitaji tena , hapana ila ni kwa kuwa siwezi kuwa na wewe tena.Ndiyo siwezi na unaweza ukajiona huhitaji kuwa na mimi na hata ikakuchukua muda mrefu hadi kuamua kuisoma hii barua ila tambua sitoweza kuwa na wewe tena ingawa nakupenda na UNANIPENDA kwa dhati mpenzi.
Unanipenda nalijua hilo na ndiyo maana umeamua kuisoma barua hii.Umedanganywa na uzuri wa Harriety, sawa ni mzuri ila Hakupendi na wala si saizi yako huyo si wa kuolewa bali wa kufanyia mauzo , naam kila mtu anampigania afanyie mauzo mtaani na ndicho akifanyacho we hujui.
Utajuaje wakati anakulevya na penzi lake na uzuri wake autumiao kama silaha kwako? Sitaki kukulaumu sana kwa kuwa najua ni wanaume wengi sana ambao wangemtamani Herriety hata mie ningemtani ningekuwa wanaume kama wewe.Siku nilipomwona mara ya kwanza nikajiona kabisa sistahili kushindana naye kukupenda ingawa baadaye nikatambua si mwanamke mwenye mapenzi kwako. Najua hujui ni lini na vipi nilikutana naye lakini naomba nikuambie ukweli huu mchungu kuwa Harriety hakuwa mwanamke mwaminifu, zaidi ya mara ya tatu nimemshuhudia akigombanisha wanaume kwa sababu ya usaliti wake.
Matilaba ya barua yangu si kukuambia kasoro za mpenzi wako Harriety bali ni kukuambia kuwa nakupenda na nakukumbuka pia ingawa siwezi kuwa na wewe , unajua kwanini? Nadhani hujui ingawa utakuwa unabashiri, ngoja tuu nikwambie ukweli Herriety namfahamu na nimekua naye na kucheza naye.Likizo zote tumekuwa tukishinda pamoja na alikuwa akijua wewe ni mpenzi wangu na nilikuwa nikimjua mwanaume aliyekuwa akimpenda sana ingawa tangu zamani uzuri wake umemfanya ashindwe kuikwepa mitego aliyokuwa akitegewa na wanaume "mifisi" yenye tamaa kama wewe na kujikuta akijihusisha na wanaume wengi kimapenzi bila kupenda hatimaye akaamua kuendelea na tabia hiyo.
Katika kuumia kwangu baada ta kukukosa nikaamua kumuumiza kwa kutembea na mwanaume ambaye alimpenda kwa dhati,kitendo kilichoharibu maisha yangu kwani licha ya kupata kisonono na Virusi vya UKIMWI nilikutana na kipigo kitakatifu baada ya kufumwa na mwanamke ambaye naye alikuwa akimpenda zaidi ya Herriety leo hii ninapoandika nipo Hospitalini nikijaribu kupambana na maumivu ya majeraha ya moto na visu kwani baada ya kufumwa gesti nilichomwachomwa visu vya haja na kutolewa nje nikiitiwa mwizi ambapo nikaonja kidogo maumivu ya mawe na kuchomwa kwa petroli kabla ya polisi waliokuwa doria kuniokoa. Najua utashtuka lakini kushtuka kwako hakutokiokoa na kifo kwani nisipokufa kwa mateso haya basi nikitoka hapa nitajiua maana nimetia aibu kubwa familia yangu nawe unawajua wazazi wangu.
Nikupendaye Alice, naomba usisahau kituko hiki cha mapenzi yetu ya kitoto; pale nilipokusindikiza hadi kwenu kisha nikalala chumbani kwako huku kaka yako na mdogo wako uliyekuwa ukilala naye chumba kimoja kujua. Kituko hiki hunipa tabathamu na nguvu mara chache na nikaamini unanipenda kweli.
Nilimaliza kuisoma barua hiyo kwa tabathamu, si kwa sababu ya kufurahia mateso yake bali ni kituko ambacho hata yeye kuwa katika mateso aliweza kutabathamu.Najua hata wewe unaweza kutabathamu ngoja nikuambie. Siku moja kabla ya kwenda Mwanza kujiunga na kidato cha tano nilienda hadi shuleni ambako Alice alikuwa akisoma. Ulikuwa ni mwendo wa saa kama mbili hadi mbili na nusu, lakini kwa kuwa nilikuwa nikienda kumuaga niliyekuwa nikimpenda niliona ni kama safari fupi tuu ya kwenda chooni. Baada ya kuongea hili na lile na mpenzi wangu Alice nikataka kuondoka lakini hakukubali kuniacha niende peke yangu akadai angenisindikiza kidogo.
Nami bila hiyana nikamkubalia na tukaianza safari yetu ambayo ilijaa huba kwa kuwa ilipita kwenye njia iliyokuwa msituni hivyo upweke na ukimya wa njia ulinogesha safari. Taratibu tukiwa tumeshikana mikono wakati mwingine tukikimbuzana ama kufanyia vituko mbalimbali ili mradi kukoleza huba tukajisahau na kujihisi tulikuwa tukisafiri wote na si kusindikizana tena.Baada ya saa tatu ambapo ilikuwa saa moja tukajikuta tumekaribia nyumbani kwetu. "He! imekuwaje tumefika huku?" Aliuliza baada ya kuwa hatua kama ishirini kutoka nyumbani kwetu.
"Sijui'' Nilimjibu nikitafakari cha kufanya. "Na sina ndugu hapa kijijini kwenu ningezuga hata kuumwa"Aliongea huku bado nafikiria lakini mara tukasikia sauti nilizozifahamu.Alikuwa baba yangu akipita njia ile ile tuliyokuwa akielekea nyumbani kwa babu huku akilalamika mie kutoonekana siku ile wakati nilikuwa na safari. Ni sauti aliyoitambua kwani ilifanana sana na yangu , bila kumweleza alikimbilia kwenye kichaka kilichokuwa karibu huku nikijifanya ninakimbia kuelekea nyumbani na mara nikakutana na baba. "Ulikuwa wapi?" Aliuliza akiwa na hasira.
"Nilienda shuleni kuna mtu alikuwa na picha zangu za mahafali" Nilimjibu nikimpa kibahasha ambacho nilikuwa nikiomba Mungu asikipokee na sijui ni Mungu ama shetani hakukipokea kwani kilikuwa na picha za Alice tuu hakukuwa na picha yangu hata moja. " Shika huko siku zote ulikuwa wapi?, tunakuambia mara nyingi uwe unajiandaa lakini hadi dakika ya mwisho unatuhangaisha nakwambia utaachwa hata siku ya kiyama" Alimalizia kwa utani ambao alikuwa akipenda kuutumia na kumfanya hata mama yangu aliyekuwa na hofu kubwa atabathamu kwani kosa langu lilionekana kama lake alikuwa akifokewa na baba tukikosea kama vile ndiye aliyekuwa akitutuma tukosee.
Yakaisha tukafikia sebuleni ambako tulikuta wanafamilia wengine wameshakula.Nikalamna kisha kikao cha wanafamilia kilifanyika kikiwahusisha wazazi kaka yangu mdogo wangu na dada zangu ambao walinipa baraka zao na mafunzo mengi ambayo nahisi hayakuniingia kwani nilikuwa namfikiria Alice kule kichakani alikokuwa amejificha. Saa tano usiku tukaingia kulala ambapo nilitakiwa kuwasubiri ndugu zangu niliokuwa nikilala nao chumba kimoja japo vitanda tofauti walale kisha nikatoka kwenda kumchukua Alice pale kichakani alipokuwa amekaa kwa saa tano.
Ingawa alikuwa na njaa hakutamani chakula hivyo tukaingia kwa kunyata chumbani kisha kulala hadi alfajiri sana ambapo nikamtoa hadi stendi akijifanya msafiri ama anamsindikiza mtu kisha kurudi nikisaidiwa na tabia yangu ya kufanya mazoezi kila asubuhi hivyo nilivyorudi natokwa jasho hakuna aliyenishangaa kati ya wote niliokuta wameamka tayari kunisindikiza stendi. Baada ya kuoga tukaondoka na ndugu zangu hadi stendi. Nikaangaza huku na huko bila kumuona hadi pale gari lilipokaribia kuondoka nikamwona akinipungia mkono wa kwa heri kabla ya kutupa busu lake hewani nami nikimjibu kwa tabathamu. Ni kama jana hivi lakini miaka saba imepita tangu tukio hilo la kufurahisha litokee.
Hapo nikaanza kukumbuka mambo mazuri na ya kuvutia tuliyowahi kutafana na Alice hapo zile chembechembe za huba zikachipua tena na kujiona namhitaji Alice ambaye kwa barua yake amedai alilazwa zaidi ya mwezi mzima lakini ile barua nimeisoma miaka miwili baada ya kuipokea. Nikaaamua kumpigia Harriety ambaye kugombana naye kutokana na kukosea kunitumia meseji ya mwanaume mwingine ndiko kulinifanya nimkumbuke Alice na kuisoma barua yake ambayo niliipuuza kwa miaka miwili ikiwa ndani ya bahasha bila kufunguliwa. Alipokea simu na kuwa mkali kama kawaida yake akinikosea akiamini kuwa ningepoa na kumwomba msamaha kama alivyozoea hata akikosea.Nikamuuliza kama alikuwa na taarifa zozote juu Alice.
"Kumbe unajua tunafahamiana naye? pole sana Alice alifariki mwaka juzi kwa kisa cha kusikitisha sana nasikia aliiba hivyo akachomwa moto pole sana mpenzi" Aliongea kwa sauti ambayo sikuielewa kama ilikuwa ya uchungu ama kebehi. Sikumbuki kama nilifanikiwa kukata simu na chozi likanitoka nikijiona mkosefu. Ni miezi miwili baada ya kuisoma ile barua na kupata taarifa juu ta kifo cha Alice na ni siku moja tangu nitoke kuliangalia kaburi la Alice ambaye sikumwambia neno lolote zaidi ya kumweleza kuwa BADO NAMKUMBUKA kama yeye alivyodai kwenye kuwa Ananikumbuka. Siamini Alice kipenzi changu BADO NAKUKUMBUKA NA NITAKUKUMBUKA MILELE....
No comments: