Hizi ndizo dalili za kuvunjika kwa mapenzi



Wapenzi wengi ambao wamefikia hatua ya
kuachana wameshindwa katika vipimo vya
kitalaamu kuthibitisha ubaya waliokoseana,
ambao unaweza kubeba uamuzi huo mzito wa
kuvunja ahadi zao za kimapenzi na hata ndoa.
Kwa mujibu wa watalaam wa masuala ya
ndoa na mapenzi inaelezwa kwamba wapenzi
wanaoachana huwa hawana sababu za msingi,
hii inatokana na ukweli kwamba wanaoachana
hawafahamu kiini kilichowatenganisha katika
makubaliano muhimu na ya kwanza kabisa
ulimwengu ya watu kufikia hatua ya kupeana
utu wao.
Inasemwa hivyo kwa sababu ukilinganisha
matatizo yanayotenganisha watu hayabebi
hoja zinazokubalika na wapenzi wote. Kwa
mfano kama wapenzi watasema wameachana
kwa sababu wamefunaniana na wakadhani
hiyo ni sababu wanakuwa wanaudanganya
zaidi umma kwa maana kuna
wanaofumaniana, wanaodhalilishana,
wanaotukanana, wasioheshimiana kabisa,
lakini bado wanadumu katika ndoa zao bila
kuachana.
Kwa ulinganifu huo, wachunguzi wa mambo
ya ndoa wanasema, kuachana si zao linaloota
na kukua kwa siku moja, bali ni migogoro
isiyoshughulikiwa kwa muda mrefu ambayo
huwaachanisha wanandoa taratibu bila wao
kujua.
Kwa maana hiyo wanaoachana au
watakaoachana wanatakiwa kufahamu kuwa
safari yao ya talaka haianzi na kumalizika
kwa siku moja, isipokuwa hufikia katika
hitimisho baada ya kuwepo katika mwendo
kwa muda mrefu, ambapo dalili zake huwa
hizi zifuatazo:
1 : Ikiwa mmeoana na baadaye mkaanza
kuonana ni watu msiohitajiana sana katika
maisha. (mapenzi kuchuja). Kila mtu
anafahamu kuwa wakati wa uchumba
mapenzi huwa moto moto lakini baada ya
kuoana hujitokeza hali ya kuanza kuzoea. Hii
inatokana na ukaribu ambao mwanzo
haukuwepo au kusitishwa kwa machimbezo
yaliyokuwa yakiboresha uhusiano. Kwa mfano
wapenzi wengi wanapokuwa kwenye uchumba
hufanyiana mambo mengi yakiwemo ya
kutumiana zawadi na kadi au kutoka pamoja
kwa matembezi, lakini wakioana hujikuta
hawafanyiani hayo, jambo ambalo huathiri
mapenzi yao.
Uchuchuzi unaonyesha kuwa wapenzi walio
kwenye uchumba wanapokuwa pamoja
hutumia muda mwingi sana kuomngea kwa
simu, kutumiana meseji, kuzungumza tofauti
na mume na mke. Ukitaka kuthibitisha keti
barabarani ukiona mwanaume na mwanamke
wamo ndani ya gari hawaishi kucheka na
kuzungumza wafuatilie utakuta mwisho wa
safari yao wanaagana kila mmoja anakwenda
kwake (ina maana si mume na mke hao).
Ni nadra sana kuwakuta wanaume wakiwa
pamoja na familia zao wakifurahi, jambo
ambalo hupunguza upendo na kuleta mazoea
na hisia za kutohitajiana sana. Hili halifai
likiwepo ni ishara kuwa mapenzi yanakaribia
kunyauka.
2 : Mkiwa hamsameheani na kusahau
mnapokoseana. Si watu wengi ambao wako
tayari kusamehe na kusahau makosa.
Wapenzi wa dunia ya leo wakisema
nimekusamehe haina maana wamefuta kosa
bali hiliweka kando na kulikumbushia wakati
mwingine. ‘Hili ni kosa la tatu tarehe fulani
ulinifanyia hivi, wiki iliyopita na jana
kulinijibu hivi hivi sasa leo siwezi
kukuvumilia”
Kauli kama hizi hutoka kwenye vivywa wa
watu ambao hawako tayari kusamehe, kosa la
mwaka juzi litakumbushwa tena na tena na
kuzidi kuchochea ugomvi hata uliokuwa
mdogo na kuoneka mkubwa kwa sababu tu
umehusishwa na makosa yaliyopita.
Inashauriwa kuwa uhai wa mapenzi lazima
uambatana na kusameheana kama wanadamu
na kusahau makosa. Hili lisipofanyika ni rahisi
kuua penzi na kuwafanya watu kuachana. Ni
vema kila mmoja wetu akajichunguza tabia
yake na kuacha kukumbusha makosa
yaliyopita.
3 : Msipokubali kuwekeana mipaka ya
kiutawala. Kuna suala linatambulishwa sana
siku hizi na wanaharakati, linaitwa usawa wa
kijinsia, jambo hili limekuwa likichangia sana
migogoro ya ndoa hasa baada ya kutumiwa
vibaya na wahusika. Hakuna ubishi mila za
kiafrika zinaongozwa na mfumo dume,
kuubadili mfumo huu kwa haraka kumekuwa
kukiharibu uhusiano mwingi wa kimapenzi
kutokana na ukweli kwamba ni wanaume
wachache sana ambo wako tayari kuishi na
wanawake wanaovutana nao kimamlaka.
Hivyo ili kunusuru hili lisiwe kikwazo katika
mapenzi tunashauri kila mwanandoa
kuheshimu mipaka yake na kujali zaidi utu na
si usawa kama inavyotambulishwa (haya ni
mawazo yangu). Watu wanaojali utu katika
familia watakuwa tayari kuwapa heshima
wanaoishi nao kwa kusikiliza mawazo yao na
kutokutumia nguvu kuwakandamiza wengine.
Ni vema mwanamke akachungua nafasi yake
kwa mumewe na mume naye akamuheshimu
mke kwa utu wake.
4 : Msipozungumzia vikwazo vya maisha.
Matarajio ya watu wengi wanapokuingia
katika uhusiano wa kimapenzi huwa ni
kupata faraja, ni wachache kati yao hufikiria
kukutana na vikwazo vya kimaisha.
Tafiti zinaonyesha kuwa wakati mtu
anapotafuta mpenzi huamini toka moyoni
kuwa akiwa na waridi wake matatizo ya
upweke, kukosa msaada wa hili na lile
yatakwisha lakini baadaye anakuja kubaini
kuwa aliyokusudia kuyapata hayapati tena na
hivyo kujuta kwa kauli kama hizi. “Kama
ningejua kama mwanaume mwenyewe yuko
hivi nisingekubali kuolewa.”
Kauli kama hizi mara nyingi hutokea kwa
watu ambao hawazungumzii matatizo na
vikwazo wanavyokutana navyo katika
mapenzi na kuviondoa.
Kama mpenzi wako ana matatizo unasubiri
nini kuyatafutia ufumbuzi au kama maisha
hayaendi sawa ukimya wa nini kwa mwenza
wako, kaeni chini muambizane kuwa
mnaupungufu wa fedha na dhiki kadhaa wa
kadhaa, ili kama kutatokea kukosa mahitaji
muhimu liwe ni jambo linaloeleweka na wote
kuwa linatokana na kipato kushuka.
Uchunguzi unaonyesha kuwa wanaume wengi
wanapokukwama kiuchumi hupunguza
matumizi kimya kimya jambo ambalo
huwafanya wanawake wengi kubaki
wakitumikia zana potofu kuwa huenda
wananyimwa baada ya kuwepo kwa nyumba
ndogo.
5 : Msipokuwa na mipango ya pamoja na
uwazi wa matumizi ya pesa.
Nina ushahidi wa kutosha juu ya kuwepo kwa
wapenzi hasa wenye kipato kutokuwa wawazi
katika mipango yao ya kimaisha na matumizi
yao pesa. Natambua baada ya kufanya
uchunguzi wangu kuwa pesa za baadhi ya
wanawake huwa hazina matumizi ya wazi,
badala yake wanaume hubanwa kwa
kisingizio kuwa wao ndiyo wana wajibu wa
kutunza familia.
Hali hii imekuwa ikileta migogoro mingi sana
kwenye familia na kushusha upendo kwa vile
upande unaohudumia familia hapa haijalishi
mume au mke huwa unajikuta ukikereka kwa
kukosa msaada wa upande wa pili na hivyo
kuondoa mapenzi ya kweli.
Kama hilo halitoshi vijana wengi wa kiume
siku hizi wamejikuta wakiahirisha mapenzi
yao kwa wasichana baada ya kukosa
ushirikiano wa kimapato na matumizi yake.
“Ninashida ya kuonana na wewe mpenzi
wangu, vipi nikufuate kazini?” Jibu linakuwa
“Hapana niko bize sana leo.” Inawezekana
kabisa mtu akawa hayuko bize lakini kwa
sababu anaogopa kukamuliwa kipato na yeye
mambo yake hayako sawa anaamua kukacha
ahadi. Lakini ukiwepo ushirikiano wa
kimatumizi husaidia kudumisha mapenzi.
Inashauriwa kwamba kama wapenzi wote
wana kazi na wanapokea mishahara ni vema
vipato vyao vyote vikatumika katika kutunza
na kuendeleza familia. Tabia ya mwanamke
kumtegemea mwanamume kimatumizi huku
yeye akitumia pesa zake kwa manunuzi ya
vipodozi na nguo au kufanyia mambo yake
kwa siri haijengi badala yake inanyausha
mapenzi kama siyo kuyaua kabisa.
6 : Mkiacha kujaliana na kupeana haki katika
tendo la ndoa.
Tendo la ndoa ni muhimu kwa wanandoa kwa
vile linahusika na hizia za mwili. Matatizo
mengi ya usaliti kwa mujibu wa uchunguzi,
yanatokana na wapenzi kutotoshelezana
wakati wa tendo la ndoa. Kwa kutokutambua
madhara au kwa uzembe, wapenzi wengi
wamekuwa wakiacha kutimiziana tendo hilo
bila kuwepo kwa sababu za msingi. “Mimi
nimechoka siwezi kufanya mapenzi.”
Inawezekana kweli mtu akawa kachoka sawa
na kauli hiyo lakini sababu hiyo haiwezi
kumfanya mwenza akazimaliza hisia zake,
isipokuwa kwa kutafuta njia mbadala
zikiwepo za usaliti. Sambamba na hilo
wapenzi wengi wamenyausha mapenzi yao
kwa kutokuwa wabunifu katika uwanja wa
sita kwa sita kwa kutokujituma, kutobuni
staili mpya, kutochombeza na kutohamasisha
kwa cho chote na kibaya zaidi kutokuwepo
kwa usafi wa mwili yao.
Katika kipindi cha maisha yangu ya ushauri
wa masuala ya saikolojia, maisha na mapenzi
nimekuwa nikikutana na wanaume wengi
wanaolalamika kuwa wana upungufu wa
nguvu kiume.
Lakini wengi kati ya hao ambao mamia yao
nimeshawasaidia walijikuta wakipungukiwa
nguvu zao kwa sababu za kisaikolojia
zilizochochewa pia na udhaifu wa wenza wao.
Kama utakuwa na mtu kwa mfano, ambaye
mtakutana naye chumba kile kile, eneo lile
lile, staili zile zile, kwa miaka mitano
mfululizo bila shaka hali ya kukinaishwa
itakuwepo na hivyo mapenzi kunyauka.
Katika hili ni vema kujifunza zaidi namna ya
kutoshelezana katika tendo la ndoa.
7 : Mkibeba fikra binafsi kwa kila mtu kutaka
mafanikio yake.
Maisha ya wapenzi wengi yamekuwa
yakipoteza maana kiasi cha kufikia kuchuja
kutokana na wapenzi wenyewe kuwa na
mawazo ya ubinafsi. Utakuta watu wameoana
lakini kila mmoja anakabili changamoto za
maisha peke yake, hali ambayo humfanya
atumie nguvu kubwa kutafuta ushindi wa
matatizo yake.
Mantiki ya maisha ya ndoa ni kusaidiana.
‘Mungu alimwambia Adamu kuwa atampatia
msaidia wa kufanana naye ambaye ni
mwanamke aliyeitwa Hawa.’ Upo pia msemo
usemao ‘Kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi’
Ni wajibu wa wanandoa kuhakikisha kuwa
maisha yao yanakuwa ya nyuzi mbili ili
yasikatike upesi. Lakini ikiwa kila mtu
anajenga nyumba yake, anafanya biashara
zake, ana mipango yake binafsi ujue mwisho
mbaya wa mapenzi umesogea.
8 : Mkiwa watu wa kutoa siri zenu nje.
Upo udanyanyifu mwingi wa kimawazo
miongozni mwa wapenzi wengi kiasi cha
kudhani kuwa kumwambia rafiki au ‘shoga’
masuala ya ndani ya ndoa ni kutafuta suluhu
ya matatizo. Hii si sahihi kwa vile upo
ushahidi mkubwa juu ya wapenzi wengi
ambao walijikuta katika wakati mgumu baada
ya kutoa siri zao nje. Ifahamike kuwa ndoa
imara ni ile inayoheshimika katika jamii, na
heshima hiyo haiwezi kuwepo kama
wanandoa hawatakuwa makini katika kutunza
siri za mapenzi yao.
Haipendezi kwa mwanamke/ mwanaume
kwenda kijiweni na kuanza kuanika mambo
ya ndani kwa mfano. ‘Yaani leo mume wangu
hakuacha kitu chochote ndani sijui itakuwaje.
‘Sema wanawake wote lakini si mke wangu,
ana kasoro nyingi sana.’
Kauli kama hizi na nyingine ambazo zinatoa
nje udhaifu wa maisha yenu hazifai, kwani
katika kila ndoa kuna udhaifu mwingi
ukiwepo ukimya ina maana wahusika
wanaweka udhaifu wao kifuani kwa maslahi
ya maisha yao. Na wewe uwe hivyo kwa
kutunza siri za mumeo.mkeo.
9 : Msipokuwa wawazi katika kuzungumzia
upungufu wa kibinadamu mlionao na
kusaidiana.
Wapenzi wasomaji wangu, hakuna
mwanadamu aliyekamili kwa asilimia mia
moja. Ukimuona hodari wa hili ni dhaifu wa
lile, kinachotakiwa ni kusaidiana katika
kufikia ukamilifu. Faraja inayopatikana katika
upungufu wa mwanadamu hasa usiokuwa wa
kimaumbile ni kuwepo kwa utatuzi wake.
Kuna wapenzi wengi wamefikia kuachana
kwa kasoro ndogo ndogo kama za kutojua
mapenzi, au hata uchafu wa mwili ambao
kama wangekaa na kujadiliana pamoja
wangepata ufumbuzi wa tatizo.
Inashauriwa kuwa kunapokuwepo upungufu
wowote wa kati ya mwanaume na mwanamke
ni wajibu wa wapenzi wenyewe kukaa chini
na kuelezana wazi na kushirikiana katika
kupata ufumbuzi. Unashindwa nini kuwambia
mpenzi wako kuwa hakutoshelezi katika
tendo la ndoa, ana harufu mbaya mwilini,
mchafu, hajui mapenzi na mambo kama hayo!
Kikubwa katika hili ni kujua namna ya
kuwasil;isha ujumbe, maana kuna wengine
hawana lugha nzuri za mawasiliano “Yaani
mke wangu unanuka sana mimi nakerwa
sana” Ukisema hivi utamfanya mwenzako
aone kama unamnyanyapaa. Tumia lugha
nyepesi itakayosaidia kumaliza tatizo msikae
kimya bila kuzungumzia upungufu wenu
mtajikuta mnaachana.
10 : Mkiendekeza nguvu katika kutwaa
madaraka ndani ya familia.
Kuna baadhi ya familia kila mmoja ni mtemi
hakuna diplomasia katika kutatua migogoro.
Utakuta mwanamke ni mbogo na mwanaume
naye ni simba, basi shughuli inakuwa nzito.
Ndoa inakuwa uwanja wa ndodi kila siku
kutoana manundo.
Hakuna mapenzi ya namna hiyo! Kanuni za
mapenzi bora zinakataza wapenzi kutumia
nguvu kutwaa madaraka au haki ndani ya
familia. Inawezekana kabisa wewe kama mke/
mume ukwa na haki katika jambo fulani
lakini haki hiyo haikupi fursa ya kutumia
nguvu nguvu kuipata.
Kinachotakiwa katika mapenzi ni
kuheshimiana, kwani katika hali ya kawaida
utumiaji wa nguvu katika kudai haki ndani ya
familia ni moja kati ya mambo yaliyoshindwa
katika historia kuleta maelewano. Kama
unadhani naongopa keti chini ujitathmini
tangu umeanza kumchunga mumeo/mkeo na
kumbana kwa ngumi umepata mafanikio gani,
ameacha tabia yake au ndo anazidi?
Umwamba haufai kutumika katika maisha ya
ndoa kwa mtu yoyote awe mwanaume au
mwanamke.
11 : Mkiwa watu msioheshimiana mbele za
watu na kupenda zaidi kusema kuliko
kusikiliza.
Nimeshuhudia wapenzi wengi ambao hawajui
umuhimu wa kuheshimiana mbele za watu.
Utakuta mwanamke/mwanaume akimwaibisha
mwenzake mbele za watu kwa kumfokea,
kumwita jina baya, kumtusi, kumtoa kasoro
na hata kumdhalilisha. Kitendo hiki ni kibaya
na maumivu yake hudumu kwa muda mrefu
akilini mwa mtendewa.
Inashauriwa kwamba wapenzi wanapokuwa
mbele za watu wachunge ndimi zao na wawe
watu wanaopenda zaidi kusikiliza kuliko
kunena. Inaelezwa, penye wingi wa maneno
yapakosi kuwa na uovu. Kuna wanawake
wakianza kuwatusi waume zao mpaka
nyumba ya 50 wanasikia au wakati mwingine
hutoka nje na kumwaga mitusi kana kwamba
wameambiwa watapewa tuzo. Hiyo si
heshima na hajawahi mtu kuheshimika
kwenye jamii kwa uhodari wa kutukana watu.
12 : Msipokuwa tayari kukubali kosa na
kujirekebisha.
Dalili nyingine ya mapenzi kunyauka ni kwa
wapenzi wenyewe kuwa na tabia ya
kutokukubali makosa na kujirekebisha.
Utakuta mwanaume/,mwanamke
ameshaambiwa mara nyingi na mwenza wake
juu ya tabia zake na pengine hata marafiki
zake wamemtahadharisha lakini habadiliki,
kila siku anarudia makosa yale yale ambayo
yanamuumiza mpenzi wake. Huu ni
mwenendo mbaya, ubinadamu unamtaka kila
mtu kuwa tayari kukiri kosa na kujirekebisa
13 : Msipokuwa watu wa kuitafuta furaha
pale inapokosekana.
Wakati mwingine harakati za maisha huleta
huzuni, kwa mfano, kama wanandoa
watafiwa, kuuguza, kufukuzwa kazi, kupoteza
mali kwa kuibiwa na matukio kama hayo
huondoa furaha. Hapa inashauriliwa kwamba
endapo furaha itaondoka kwa sababu yoyote
wanandoa wanajukumu la kuitafuta. Hapa
namaanisha kutiana moyo na kuwezeshana
kusonga mbele wakiamini kuwa hakuna
marefu yasiyokuwa na ncha. Kuacha huzuni
itawale nyumba yenu kwa muda mrefu
hupunguza mapenzi.
14 : Msipozingatia kuombana msamaha bila
kujali nani mwenye kosa.
Kuombana msamaha ni jambo la lazima kabisa
katika ndoa, na busara inamtaka mwenza
kuwa tayari kuomba masamaha hata kama
anaona kabisa hakuna kosa la msingi
alilolifanya mbele ya mwenzake.
Kung’ang’ania kutaka haki kipindi cha
kuzozana ni njia ya kuelekea kukosana zaidi
na hatimaye kuachana. “Nakuomba unisamehe
mke/mume wangu, najua nimekuudhi.” Baada
ya kutoa kauli hiyo na mzozo kupoa mhusika
anaweza kufafanua kilichotokea na hapo
anaweza kueleweka zaidi kuliko kipindi
ambacho mpenzi wake anakuwa na hasira.
15: Msipokuwa tayari kukumbushana wajibu
na mwenendo wenu
“Atajijua mwenyewe siku yakimkuta ya
kumkuta huko ndo atafahamu” “Mimi
nimechoka nimebaki namwangalia tu.” Kubaki
unamwangalia mpenzi wako anaharibikiwa si
uamuzi wa busara kwani mwisho wa siku
kama ni aibu itakufikia na wewe pia.
Ukimuona mwenzako anakwenda nje ya
mstari wa jamii mrejeshe na kuzidi
kumkumbusha kila siku wajibu wake kama
baba au mama wa familia, hii inasaidia
kumuweka sawa mahali anapokosea.



No comments:

Powered by Blogger.