Simu Ya Mwenza Wako ya Nni Unajipa Presha Bure


KWA wanandoa, uaminifu limekuwa ni jambo la msingi sana ndiyo maana kila siku tunasema, ili udumu na huyo uliyeingia naye kwenye ndoa, mjengee imani kuwa wewe ni wake na haitatokea siku ukamsaliti. Lakini wakati ukweli ukiwa hivyo, kwenye baadhi ya ndoa kuna sarakasi nyingi sana. Katika ulimwengu wa sasa kumekuwa na tatizo kubwa la baadhi ya wanandoa kutibuana kila siku kisa kikiwa ni kutokuaminiana kupitia simu zao. 

Kwa hili niseme tu kwamba, ni wanandoa wachache sana ambao wanaamini simu za wenza wao hazina madhambi, wengi wanahisi wanasalitiwa kupitia simu na ndiyo maana unaweza kukuta mke akishika simu ya mumewe tu inakuwa shida. Si hivyo tu, wapo wake za watu nao hawataki kabisa simu zao zishikwe na waume zao, unajiuliza kwa nini iwe hivyo kama kila mtu anajiamini? Lakini sasa, leo naomba niwashauri kitu wale walioingia kwenye ndoa. Kuna mambo ambayo unatakiwa kuyapuuza laa sivyo huwezi kuwa na amani katika maisha yako. 

Kama kweli unampenda huyo uliyenaye, usimfikirie vibaya! Jenga imani kuwa, hawezi kukusaliti. Hii tabia kwamba simu ya mwenza wako ikiita tu unachungulia kujua nani kapiga, SMS ikiingia unafungua, ya nini kujipa presha? Hivi unadhani kweli unaweza kumzuia huyo mwenza wako asikusaliti kwa kutompa uhuru wa simu yake? Hili ni gumu hivyo unachotakiwa kufanya ni kumuacha na simu yake. Usijipe presha zisizo na msingi. Unaweza kukurupuka, ukapokea simu ya mumeo, mara unakutana na sauti nyororo ya msichana, presha inakupanda bila kujua aliyepiga ni nani. Na yeye kwa kuwa aliyepokea siye aliyempigia, anakata. 

Wewe huko uliko unachanganyikiwa, unafikiri aliyepiga ni mchepuko. Kumbe aliyepiga labda ni mfanyakazi mwenzake au rafiki yake wa kawaida tu. Wewe unakuja juu na kumwambia mumeo anakusaliti, kumbe hamna kitu kama hicho. Au wewe mwanaume unaweza kuchukua simu ya mkeo, ukaenda kwenye sehemu ya meseji ukitaka kujua ni nani huwa anachati nao. Bahati mbaya unakutana na meseji ya kimahaba iliyotumwa na mwanaume ambaye alikosea namba. Wewe bila kuwa na uhakika na kile ulichoona unakimbilia kuhitimisha kuwa, mke si muaminifu. Hili ni tatizo kubwa ndiyo maana leo kupitia safu hii nimeona niwakumbushe tu kwamba, simu ya mwenza wako achana nayo ili kujihakikishia amani ya moyo.



No comments:

Powered by Blogger.