CHANGAMOTO YA KUMFUMANIA UMPENDAYE NA HATARI 5 ZA KUMUACHA



KATIKA maisha ya kimapenzi yapo mengi ya kuvumilia ili kuweza kudumu na huyo uliyetokea kumpenda. Hata hivyo kuna ambayo kuyavumilia inahitaji ujasiri wa hali ya juu.

Hebu vuta picha, unaingia kwenye uhusiano na mtu ambaye moyo wako unaamini ni mpenzi sahihi, unampenda, unamheshimu na kumjali lakini siku moja unamfumania na mtu mwingine. Hivi kama ni wewe utaumia kwa kiwango gani?

Ninavyojua maumivu yake hayaelezeki lakini ukae ukijua kwamba, wakati ukihisi maumivu ni makali sana, wapo ambao wanawafumania wapenzi/ wanandoa wenzao na kuamua kusamehe. Kwa nini wanafanya hivyo? Wanajua madhara ya kuacha baada ya kufumania.

Huenda wewe hujui na siku zote unadhani ukishamfumania mwenza wako suluhisho ni kumuacha. Sipingani na uamuzi huo ambao baadhi watu wamechukua lakini wataalam wa mambo ya kimahusiano hawashauri hivyo.
Ndiyo maana nimeona leo kupitia ukurasa huu nielezea kwa ufupi hatari tano za kumuacha uliyetokea kumpenda sana baada ya kumfumania.

Utamuota kila siku
Ifahamike kwamba, si kila anayekusaliti hakupendi na si kila unayemuacha humpendi. Wapo ambao wanasaliti lakini mapenzi yao kwa wenza wao yako palepale.
Kwa maana hiyo ukimuacha mtu ambaye huenda ana mapenzi ya kweli lakini ‘shetani kampitia’, hatakauka ndotoni mwako.

Atakuwa akikusumbua sana kwani huenda unampenda sana lakini uamuzi wako wa kumuacha haukuwa suluhisho. Kwa kifupi hawezi kuondoka haraka akilini mwako.
Watakurusha roho
Wapo ambao mpaka sasa wanaumia baada ya kuwaacha wapenzi wao pale walipowafumania. Kwa mfano, ukimfumania mkeo na jamaa, kisha ukampa talaka, tambua huyo mkeo hawezi kwenda kwa mtu mwingine. Lazima atabaki na mwanaume aliyefumaniwa naye.

Kitakachotokea sasa, kila utakapowaona utaumia na wao lazima watakurusha roho. Hakuna kitu kinachouma kama kumuona mkeo wa zamani akiwa na mwanaume mwingine tena akionekana mwenye furaha zaidi.

Lazima utayumba
Huwezi kuwa sawa kwa kumuacha mpenzi wako ambaye huenda mlishakuwa na malengo makubwa maishani. Hata kama kosa alilolifanya ni kubwa lakini lazima utayumba kimaisha kwani waswahili wanasema; wawili ni wawili tu.
Kama wewe ni mwanamke utakuwa na kazi nzito ya kumtafuta mwanaume ambaye ni sahihi na wakati mwingine unaweza kuona wanaume wote ni wasaliti. Kitu hiki kinaweza kukufanya ukachelewa kumpata mbadala na hatimaye kujikuta ukiwa mpweke kwa muda mrefu.
Kuna wakati utajuta
Kama kweli mwanaume uliyemfumania ulikuwa ukimpenda kwa dhati, ni lazima kuna siku utajuta kwa kumuacha. Utajuta kwa kuwa utahisi ungeweza kumsamehe na mkaendelea kuwa pamoja.
Tena utajuta zaidi pale ambapo utakwenda kudondokea kwa mwingine ambaye ni kiwembe kuliko hata uliyemuacha.

Utateswa na vingi viulizo
Siku zote kama wewe ni mwanaume, ikatokea mkeo au mpenzi wako akachepuka na ukamkuta na mwanaume mwingine, kwanza utajiuliza kilichomfanya akusaliti?

Je, humfikishi pale anapotaka? Je, ameshawishiwa? Je, hakupendi? Je, humtimizii mahitaji yake? Hakika utakuwa na maswali mengi ambayo huwezi kupata majibu yake kwani utakuwa umeshamuacha.
Uzuri wa kumsamehe na kuendelea naye baada ya usaliti ni kwamba, mkitulia anaweza kukuambia kilichomsukuma yeye akusaliti. Kama wewe ni chanzo, utajua jinsi ya kubadilika na hatimaye kudumisha uhusiano wenu.
Ndiyo maana niliwahi kuandika kuwa, endapo siku moja utamfumania mwenza wako, usimpige wala kumuacha. Chukulia kama ni changamoto katika maisha yako.
Unajua kwa nini nasema ni changamoto? Ni kwa sababu mpenzi wako ambaye mmekuwa mkioneshana mahaba motomoto hawezi kukusaliti bila sababu. Kuendelea kuwa naye, utagundua sababu na utaweza kuifanyia kazi.
Labda iwe umekuwa ukimfumania kila mara, hapo ndipo uamuzi wa kumuacha hauepukiki.
Kwa maana hiyo, ukimfumania mpenzi wako kwa mara ya kwanza, akaonesha kujutia kitendo hicho na kuonesha dhamira ya kutaka kuendelea kuwa naye, msamehe kisha fanya kila uwezavyo ujue sababu ya yeye kukufanyia kitu hicho cha kukuumiza.
Lakini ukimfumania kisha akaonesha kiburi f’lani huku akiwa mgumu kuomba msamaha, huyo tambua siyo mtu sahihi. Alikuwa akitafuta sababu ya kuachana hivyo huna sababu ya kuendelea kumkumbatia. Ukimkumbatia ujue kabisa kusalitiwa itakuwa ni sehemu ya maisha yako.



No comments:

Powered by Blogger.