Hizi Hapa Sababu Kuu za Wanaume Kupenda Wake za Watu.



Unaendeleaje na mishughuliko yako? Mimi mzima, namshukuru Mungu kwa kunijaalia kuwa miongoni mwa wale wanaopendwa. Yes, mimi napendwa na hiyo ni bahati sana.

Wapo watu wanatafuta watu wa kuwapenda lakini mpaka sasa hawajawapata. Ndiyo maana nilishawahi kusema kwamba, ukibahatika kumpata mtu anayekupenda na kwa bahati nzuri na wewe ukawa na chembechembe za mapenzi kwake, shukuru Mungu na mshikilie.

Kumbuka mapenzi ndiyo yanachukua nafasi kubwa kwenye maisha yetu. Hata kama umzuri, una pesa nyingi na mali za kumwaga kiasi gani, kama huna mtu wa ‘kuinjoi’ naye, maisha yako lazima yatakuwa ni yenye upungufu mkubwa.

Ndiyo maana wapo ambao ni matajiri lakini kwa kuwa mapenzi yanawachanganya, wanafikia hatua ya kujiua. Hapo ndipo unathibitisha kwamba, mapenzi yanachukua asilimia kubwa katika maisha yetu ya furaha ya kila siku.

Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nataka kuzungumzia sababu tano za kwa nini baadhi ya wanaume wanapenda sana kuwa na uhusiano na wapenzi wa watu.

Nimefikia hatua ya kuandika makala haya kwa kuwa, kila siku tunasikia fulani kafumaniwa na mke wa mtu au fulani anatembea na mpenzi wa mtu. Pia wapo wanawake ambao wameingia kwenye ndoa lakini bado wanasumbuliwa sana na wanaume.
Related image
Mbaya zaidi wanaume hao wanaelezwa kabisa kuwa, wameingia sehemu ambayo tayari mwingine kashajiweka lakini hawakubali, wanang’ang’ania.

 Achilia wapenzi tu, wapo pia wake za watu ambao wanatokewa na wanaume. Yaani mwanaume anajua kabisa huyu ni mke wa mtu na anampenda sana mumewe lakini jamaa linang’ang’ania lipewe nafasi kwa kuwa lishapenda.

Katika hili naomba niseme kwamba, si kila anayemtongoza mke wa mtu au mpenzi wa mtu ni kiwembe. Wapo ambao wana mapenzi ya kweli na wameshindwa kujizuia. Mwanamke anaweza kuwa ndani ya ndoa lakini akawa ameolewa na mwanaume ambaye siye aliyepangiwa na Mungu.

Katika mazingira hayo ndiyo unamkuta mtu anakomaa na mke wa mtu, kila siku anaimbisha akiomba apewe nafasi. Akiambiwa, ‘si unajua mimi mke wa mtu’ anasema, ‘sasa mimi nifanyeje wakati nahisi wewe ndiye mke wangu niliyepangiwa na Mungu?’

 Kwa bahati mbaya zaidi unaweza kukuta na mwanamke naye licha ya kwamba ameolewa lakini naye anajihisi kumpenda mwanaume huyo na wakati huohuo hapati kile ambacho alikitarajia kwenye ndoa yake. Hapo ndipo unamkuta mwanamke anakuwa njia panda.

Anyway, hiyo ni mitihani katika maisha, sasa nirudi kwenye zile sababu za baadhi ya wanaume kuwatokea wake/wapenzi wa watu.

 PENZI LA DHATI

Kama nilivyosema, baadhi ya wanaume si kwamba wanaonyesha kuwa wao hawajatulia kwa kuwatokea wake za watu. Baadhi yao penzi la dhati walilonalo dhidi ya wale ambao wameshaingia kwenye ndoa ndilo huwasukuma kufanya hivyo.

Wanachokifanya wao ni kueleza hisia zao bila kujali kuwa, mlengwa ana mtu au laa. Ndiyo maana mtu huyo anaweza kuwa anajua ukweli kwamba fulani ni mke wa mtu lakini kwa kuwa anaamini huyo ndiye wake, analazimika kujaribu zali.

Mimi niseme tu kwamba, kwenye hili siyo dhambi kueleza hisia zako lakini ndugu yangu kama unajua kabisa huyo uliyempenda yuko ndani ya ndoa yake au ana mpenzi wake, pambana na hisia zako. Jizuie kwani kumpa usumbufu mke wa mtu ni kujitafutia matatizo bure.

HAKUNA GHARAMA

Baadhi ya wanaume wanawatokea wake za watu kwa kuwa hawatapata usumbufu wa pesa za matumizi, vocha, mavazi na vitu vingine. Wao wanaamini watakuwa wanatoa penzi tu lakini mambo mengine mwenye mke atahudumia.

Lakini wengine wanataka kuanzisha uhusiano na wake za watu kimaslahi. Kwamba mwanaume anaweza kuona mwanamke flani ameolewa na mwanaume mwenye nazo lakini mke anaonekana kutopata penzi analolihitaji. Yeye anatupa ndoano, akiamini akimridhisha kimapenzi, atakuwa anahongwa yeye na maisha yake yatakuwa poa.

Hata kwenye hili nikupe tahadhari. Kama unatokea kumpenda mke wa mtu ili umchune au ili kukwepa kugharamia, tamaa yako hiyo itakuponza. Acha utegemezi, mwanaume aliyekamilika ni yule mwenye uwezo wa kumtunza mtu anayempenda, usikimbie majukumu na kutaka vya mteremko. Kumbuka wengi walioingia kwenye uhusiano na wake za watu kwa tamaa za pesa na mali, yamewakuta makubwa.

 USUMBUFU HAKUNA

Kuna wanaume ambao hawapendi kusumbuliwa kwa mambo ya wivuwivu na wapenzi wao, mara nyingi mwanaume anapoanzisha uhusiano na mtu ambaye ana mtu wake anahisi hatasumbuliwa.

Yale mambo ya; ‘uko wapi baby’, uko na nani, nataka tuonane leo’ yanakuwa si kwa kiwango kile ambacho kinakuwepo kwa mtu ambaye hana mtu.

 HAKUNA KUGANDANA

Wapo wanaume ambao wao wanataka kila mwanamke mzuri bila kujali ameolewa au yuko singo. Lakini pia wapo ambao hawataki kuingia kwenye uhusiano na mwanamke ambaye atagusia future. Kwa kifupi wanaume wa staili hii wanaamini wakiwa na wake za watu, hawawezi kugandwa wala kuulizwa juu ya ‘future’.

 SIFA TU

Kama ulikuwa hujui wapo wanaume ambao wakitembea na mke wa mtu wanaona sifa sana. Akimtongoza mke wa mtu, akakubaliwa, roho yake inakuwa fresh. Na wengine hawawezi kubaki na siri, kila atakayekutana naye atamwambia; ‘yule mbona nishampitia’.

Hiyo yote sifa. Mtu yuko tayari kutumia gharama yoyote ili mradi atembee na mke/ mpenzi wa mtu, aandike historia kwamba fulani licha ya kwamba ni mke wa mtu lakini ameshatembea naye.

Mpenzi msomaji wangu, leo niishie hapo lakini nilichotaka ni kueleza tu sababu za kwa nini baadhi ya wanaume wanakuwa wasumbufu kwa wake za watu bila kujali hatari iliyo mbele yao. Nasema hatari kwa sababu kumpenda mke wa mtu, ukawa unamsumbua kila wakati hatari yake ni pale taarifa zitakapomfikia mwenye mali. Yatakayokukuta hapo ni aidha kuuawa au kufanyiwa vitendo vya kudhalilishwa. Ndiyo maana hapo kati nimesema kwamba, pambana na hisia zako. Kumbuka ule usemi usemao, mke wa mtu ni sumu!


No comments:

Powered by Blogger.