Dalili za Kabla ya Hedhi

Image result for dalili za kuingia kwenye hedhi
Bassa mussa 0765203999
Mwenendo wake ni wenye kubadilika-badilika na hauwezi kujulikana kimbele jinsi utakavyokuwa. Wakati mmoja yeye yu tayari kukubali mambo; na wakati mwingine yeye ni mbishi. Yeye hutamka maneno ya kuonyesha hali ya kukata tamaa. Yajapokuwa maonyesho yako yenye kufariji, yeye huitikia vibaya kwa yale usemayo na yale ufanyayo. Yaelekea jambo dogo hufanywa liwe kubwa mno na kusababisha bishano kali. Baada ya siku chache, au juma moja hivi, mwanamke huyu “mwingine” atoweka kwa ghafula, na kwa mara nyingine tena arudia hali yake ya kawaida . . . kwa muda fulani.
KWA kweli, si wanawake wote wanaokuwa na mabadiliko hayo makubwa ya hali ya moyoni. Hata hivyo, kabla ya hedhi kuanza, huenda baadhi ya wanawake wakawa wametambua kuwa na nyutu hizo mbalimbali ndani yao. Ni nini kisababishacho mabadiliko-badiliko hayo katika hali ya moyoni? Je, kwa kweli mwenendo huo ni tokeo la mabadiliko wakati wa kipindi cha hedhi?
Dalili za Kabla ya Hedhi (PMS) Ni Nini?
Kulingana na gazeti American Journal of Psychiatry, wanawake wanaokuwa na “dalili zitokeazo kwa vipindi vya kawaida ambazo ni mbaya vya kutosha kuathiri sehemu fulani za maisha” na ambazo hutokea sikuzote kabla ya hedhi huenda wakawa wana dalili za kabla ya hedhi. Ingawa hakuna upimaji wa maabara uwezao kupima kitiba dalili za kabla ya hedhi, ni lazima wanawake wanaokuwa na dalili hizo wawe na kipindi cha juma moja au mawili pasipo na dalili hizo katika kila kipindi cha hedhi. Kwa ufafanuzi huu, madaktari hukadiri kwamba ni asilimia 10 tu ya wanawake wanaokuwa na dalili za kabla ya hedhi.
Matabibu wengine wana maoni tofauti juu ya dalili za kabla ya hedhi. Wao watoa hoja kwamba asilimia kubwa zaidi ya wanawake, kati ya asilimia 40 na 90, huwa na dalili za kabla ya hedhi. Wao hufafanua maneno hayo kuwa husababisha matatizo mbalimbali, kama vile kuongeza uzani, uchovu, maumivu ya viungo, maumivu ya tumbo, maumivu makali ya kichwa, wepesi wa kuudhika, maumivu ya matiti, kulia-lia machozi, kuwa na hamu ya kula chakula, na mabadiliko-badiliko ya hali ya moyoni. Dalili zaidi ya 150 zinashirikishwa na dalili za kabla ya hedhi. Wanawake, kutia na wale ambao wameacha kuwa na hedhi, huenda wakawa na dalili yoyote moja au kadhaa kati ya hizi. Hata hivyo, kwa ujumla, mwanamke huwa na dalili za kabla ya hedhi katika miaka yake ya 30. Kwa wanawake walio wengi, dalili za kabla ya hedhi ni zenye kutaabisha lakini zaweza kudhibitiwa. Katika makala hii tutakazia fikira watu hawa wanaokuwa na dalili za kabla ya hedhi zisizo mbaya sana.
Nancy Reame, mtafiti kwenye Chuo Kikuu cha Michigan, aliripoti kwamba dalili za kabla ya hedhi huonwa kuwa “tatizo la afya la kawaida” katika Marekani, lakini katika nchi nyinginezo kuna tofauti nyingi kwa habari ya aina na ubaya wa dalili. “Wengine huripoti dalili za kimwili zilizo kubwa zaidi na tamaduni nyinginezo huripoti dalili za kihisiamoyo zaidi,” yeye asema. Reame, ambaye amefanya utafiti katika Uchina, alitaja Wachina kama kielelezo. “Katika utamaduni wa Kichina kuwa na dalili za kihisiamoyo hakukubaliki.” Likiwa tokeo, yeye aliona kwamba wanawake watakazia maumivu ya tumbo waulizwapo juu ya matatizo ya hedhi.
Mianzo ya Dalili za Kabla ya Hedhi
Dalili za kabla ya hedhi zilizungumzwa mara ya kwanza na Dakt. Robert T. Frank wa New York katika 1931 katika maandishi yake “Visababishi vya Kihomoni vya Mkazo wa Kabla ya Hedhi.” Yeye aliona wanawake waliokuwa na uchovu, waliokosa makini, na waliokuwa wepesi wa kuudhika kabla ya hedhi.
Ni miaka 22 baadaye kwamba Katharina Dalton na Raymond Greene, matabibu Waingereza, walipotangaza maandishi fulani katika jarida la kitiba ambayo katika hiyo walitunga maneno “dalili za kabla ya hedhi.” Dakt. Dalton alirejezea dalili za kabla ya hedhi kuwa “ugonjwa wa ulimwengu ulio wa kawaida zaidi, na labda wa zamani zaidi.” Yale aliyopata juu ya jinsi dalili za kabla ya hedhi ziwezavyo kuathiri mwenendo wa mwanamke yalikuja kujulikana na umma katika 1980. Yeye pamoja na madaktari wengine walialikwa kupima kitiba wanawake wawili Waingereza walioshtakiwa kwa uuaji wa kimakusudi. Wao walitoa nadharia kwamba mwenendo wa mwanamke ungeweza kuongozwa na mabadiliko-badiliko ya kihomoni wakati wa kipindi chake cha hedhi. Kwa msingi wa upimaji wao wa kitiba wa dalili za kabla ya hedhi, adhabu juu ya uuaji wa kimakusudi katika kesi zote mbili ilipunguzwa. Katika uamuzi mmoja mshtakiwa alipata adhabu isiyo nzito sana ya uuaji usiokusudiwa kwa msingi wa “kutokuwa na hali ya kuchukua madaraka.”
Matukio ya mwenendo uletao uharibifu kwa upande wa wanawake, kama vile katika habari iliyotangulia, yaonekana kutokuwa ya kawaida. Kisababishi cha mwenendo huo na cha zile dalili ndogo zenye kutaabisha ambazo wanawake walio wengi huwa nazo karibu na wakati wa hedhi zaendelea kubishaniwa kwenye kurasa za majarida ya kitiba na yasiyo ya kitiba.
Je, kwa kweli mwenendo huo ni tokeo la mabadiliko-badiliko ya kihomoni ya vipindi vya kawaida mwilini mwa mwanamke? Au hilo wazo la msukosuko wa homoni pamoja na mwili wa mwanamke usiodhibitika ni ngano tu? Kuna maoni tofauti-tofauti juu ya jinsi mabadiliko-badiliko ya kihomoni yaathirivyo mwenendo wa mwanamke, ikiwa hayo huuathiri kwa vyovyote. Watafiti na madaktari wengi hukubali kwamba uelewevu mzuri zaidi wa uhusiano kati ya ubongo na homoni za ovari (kifuko cha mayai) wakati wa kipindi cha hedhi ndio ufunguo wa kujua ni kwa nini baadhi ya wanawake huwa na dalili za kabla ya hedhi.
Kipindi cha Hedhi
Karibu mara moja kwa kila majuma manne, mwili wa mwanamke huwa na kipindi kilicho kigumu sana kufahamika cha mabadiliko-badiliko ya kihomoni. Likiwa larejezewa na wengi kuwa “laana,” neno “hedhi” (menstruation katika Kiingereza) latokana na neno la Kilatini mensis, limaanishalo “mwezi.”
Ili kuanzisha kipindi hicho, sehemu ya ubongo iitwayo hipothalamasi hupeleka ujumbe kwa tezi-pituitari. Ujumbe huo upokewapo, hiyo pituitari hutoa homoni iitwayo FHS (ichocheayo ukuzi wa seli zaidi katika ovari). Homoni hiyo hupita katika damu hadi kwenye ovari na kusababisha kutengenezwa kwa homoni estrojeni. Estrojeni iongezekapo, pituitari huitikia kwa kupeleka homoni iitwayo LH (homoni ya uzazi). Homoni hiyo ya uzazi hupunguza kutolewa kwa homoni ichocheayo ukuzi wa seli zaidi katika ovari. Seli-yai moja yafikia upevuko (hatua ya kuweza kushika mimba) na kusafiri hadi tumbo la uzazi. Baada ya hiyo seli-yai kuachiliwa, homoni projesteroni yatokezwa. Ikiwa yai hilo halitungishwi, viwango vya projesteroni na estrojeni vyapungua upesi.
Bila kuwa na homoni za kuutegemeza, ukuta wa ndani wa mji wa uzazi waanza kuporomoka, kukiwa na damu, umajimaji, na kiasi fulani cha tishu (kundi la seli) kikitoka kupitia uke. Huchukua karibu muda wa siku tatu hadi saba kwa mji wa uzazi wa mwanamke kutoa kabisa ukuta wa ndani, hilo likimaliza kipindi kimoja cha hedhi. Kipindi kimoja kimalizikapo, ubongo huachilia homoni tena, hilo likiwa ishara ya mwanzo wa kipindi kipya.
Pigano Kati ya Homoni?
Wengine hutoa hoja kwamba kutokuwa na usawaziko kati ya estrojeni na projesteroni ndiko husababisha dalili za kabla ya hedhi katika mwanamke. Wao husisitiza kwamba kwa kawaida homoni hushirikiana kutimiza usawaziko mkamilifu. Ikiwa kiasi kikubwa zaidi cha homoni moja kinatokezwa kuliko cha ile nyingine, pigano hutokea, na kuudhuru mwili wa mwanamke.
Viwango vya juu vya estrojeni huenda vikawafanya baadhi ya wanawake wawe wepesi wa kuudhika. Kwa wengine, projesteroni huwa nyingi zaidi, ikiwafanya wahisi mshuko-moyo na uchovu.
Watafiti wengine hawakubali nadharia ya kwamba kutokuwa na usawaziko wa kihomoni husababisha dalili za kabla ya hedhi. Wao hutoa hoja kwamba mambo ya kisaikolojia na ya kijamii huwa na fungu kubwa katika kutokeza dalili za kabla ya hedhi katika wanawake fulani. Kichapo Patient Care, katika kuripoti juu ya visababishi vya dalili za kabla ya hedhi, chasema kwamba “hakuna tofauti zozote za waziwazi ambazo zimepatikana katika violezo, uwiano, kiasi, au wakati wa homoni za uzazi katika wanawake walio na dalili mbaya za kabla ya hedhi au wasio nazo.”
Kwa kielelezo, huenda mkazo ukaongeza mwendo wa dalili za kabla ya hedhi, huenda ukazichelewesha, au kuziongeza. Kitabu PMS—Premenstrual Syndrome and You: Next Month Can Be Different chaonyesha hivi: “Mkazo huzuia kuachiliwa kwa homoni na kiasi cha homoni kisichotosha chaweza kuongoza kwenye aina ya kutokuwa kwa usawaziko wa kihomoni inayofanya dalili za kabla ya hedhi ziwe mbaya zaidi.” Matatizo ya kitiba, ya kifedha, au ya kifamilia huenda yakaonekana kuwa mengi zaidi na kutoweza kudhibitika kabla ya hedhi.
Hofu ya Kufedheheshwa
Watafiti fulani hushikilia kauli kwamba huenda mwanamke akaonwa kuwa mfanyakazi au mfanya-maamuzi asiyetamanika sana akionyesha dalili zinazohusiana na kipindi chake cha hedhi. “Hiyo ndiyo njia ambayo jamii huhakikisha kwamba wanawake wanakaa mahali pao. Ikiwa wewe ni mdhaifu mara moja kwa mwezi, hilo lamaanisha kwamba hupaswi basi kufanya mambo hayo mazito, yenye mamlaka, ya kuongoza,” atoa hoja, msaikolojia, Barbara Sommer.
Watafiti wengine hushikilia kauli kwamba wanawake wamekubali dalili za kabla ya hedhi kwa sababu zinawaruhusu watumie hali hiyo kuwa udhuru kwa mwenendo wao. Katika mahojiano ndani ya gazeti Redbook, Dakt. Carol Tavris, mtungaji wa The Mismeasure of Woman, asema kwamba dalili za kabla ya hedhi “huruhusu wanawake waseme, ‘Nina tatizo gani la kitiba?’ si, kusema ‘Nina tatizo gani maishani mwangu linalonifanya nikose uchangamfu?’”
Katika 1985, wanawake walio matabibu wa magonjwa ya kiakili ambao wamo katika Halmashauri ya Wanawake wa APA (Shirika la Marekani la Utibabu wa Magonjwa ya Kiakili) walipinga kule kutiwa ndani kwa dalili za kabla ya hedhi katika Kitabu cha Maelezo cha APA cha Upimaji wa Kitiba na cha Kitakwimu. Ingawa dalili hizo zimetajwa katika nyongeza ya kitabu cha maelezo cha sasa (1987) kuwa “ugonjwa wa hatua ya mwisho-mwisho ya homoni za uzazi,” baraza la shirika hilo la APA limependekeza kutia ndani “ugonjwa wa kabla ya hedhi” (PMDD) katika habari kuu ya chapa ifuatayo. Kuutia ndani ya hicho kitabu cha maelezo kungeufanya uwe ugonjwa rasmi wa kiakili.
“Haupaswi hata kidogo kutiwa ndani mwomwote katika hicho kitabu kwa sababu huo si ugonjwa wa kiakili,” asema Dakt. Paula Kaplan, ambaye hapo awali alikuwa mshauri wa hilo baraza. “Wakati mwingine mwanamke achaguliwapo kuwa waziri mkuu wa sheria, yeye ataulizwa: ‘Je, umekuwa na ugonjwa wa kabla ya hedhi?’” yeye akasema.
Jitihada ya Kutafuta Ondoleo la Maumivu
Matabibu waendelea kubishania suala la dalili za kabla ya hedhi. Nadharia nyingi zinatokea juu ya kisababishi na utibabu hususa wa dalili za kabla ya hedhi. Madaktari fulani huhisi kwamba huenda kukawa na unamna-namna 18 wa dalili za kabla ya hedhi, kila moja ikiwa na dalili tofauti. Uchunguzi mmoja wa majuzi uliripoti kwamba (elementi iitwayo) zinki huenda ikawa na fungu katika kuchochea dalili za kabla ya hedhi. Uchunguzi mwingine ulidokeza kwamba ukosefu wa vitamini-Bhuenda ukawa kichochezi cha tatizo hilo, ukisababisha kadiri fulani ya mshuko-moyo katika wengine.
Matibabu kama vile utibabu wa kutumia nuru, kudhibiti usingizi, njia ya kutokeza hali ya kupumzika sana, dawa za kuzuia mshuko-moyo, na tembe za homoni projesteroni za kuingiza mwilini (bila kumeza) zinajaribiwa na wanawake wanaotafuta ondoleo la maumivu kutokana na dalili za kabla ya hedhi zenye kutokea mara kwa mara. Kufikia sasa, utibabu wenye matokeo sikuzote haujapatikana bado.
Wanawake wanaokuwa na dalili za kabla ya hedhi zisizoweza kudhibitika wanapaswa kumwona daktari. Kila hali ya kuwa na dalili za kabla ya hedhi ni ya aina yayo, na kila mwanamke astahili shauri kamili la kitiba na utunzaji unaofaa. Kwa sababu dalili za kabla ya hedhi zaweza kufanana na hali nyinginezo mbaya, kama vile ugonjwa wa tezi ya thiroidi, ugonjwa wa ngozi ya ndani ya mji wa mimba, na mshuko-moyo, uchunguzi wa kitiba ni muhimu.
Yapendekezwa kwamba kabla ya ziara ya kwanza kwa daktari, mwanamke aweke maandishi kamili au kalenda ya dalili za kimwili na za kihisiamoyo anazokuwa nazo kabla ya hedhi. Kujua siku ambazo huenda akawa na mwelekeo wa kuwa na badiliko la hali ya moyoni, wepesi wa kuudhika, au na mshuko-moyo kwaweza kumsaidia arekebishe ratiba yake kulingana na hali hizo. Kwaweza pia kumsaidia aamue kama ana dalili za kabla ya hedhi.
Huenda madaktari wakadokeza apunguze mambo yanayosababisha mkazo maishani mwake. Chakula chenye lishe na mazoezi ya kawaida yaweza pia kushindana na dalili za kabla ya hedhi. Uchunguzi mmoja wa chuo kikuu ulisema kwamba chakula chenye kiasi kikubwa cha kabohidrati (chakula chenye asili ya sukari), kilicho na kiasi kidogo cha protini kiliboresha hali ya moyoni ya baadhi ya wanawake wenye mshuko-moyo kabla ya hedhi. Mazoezi ya kawaida ya kutoa jasho au kutembea upesi wakati wa mchana huenda pia kukasaidia katika kupiga vita dhidi ya uchovu na hali ya kukosa uchangamfu.
Bila shaka, washiriki wa familia, hasa mume, waweza kusaidia. Wao wapaswa kujitahidi kuwa wenye fadhili, wenye ufikirio, na wenye uelewevu zaidi wakati kipindi cha mwanamke cha kila mwezi kinapomfanya awe na hali ngumu.
Bishano Laendelea
Wengine hudai kwamba si sahihi kuita mabadiliko ya kawaida ya kihisiamoyo na ya kimwili ambayo mwanamke huwa nayo wakati wa kipindi chake cha hedhi ‘dalili za ugonjwa.’ Na wengine hawaoni dalili za kabla ya hedhi kuwa jambo halisi, wakidai kwamba zawafedhehesha wanawake.
Hata hivyo, kwa wanawake kadhaa, dalili za kabla ya hedhi ni jambo halisi. Kila mwezi, wao huwa na dalili zinazofanya kukabiliana na familia na kazi kuwa jambo gumu. Jitihada ya kutafuta ondoleo la maumivu hayo na kupata uelewevu yaweza kuthibitika kuwa jambo la kukatisha tamaa huku matabibu wengi na wale wasio matabibu waendeleapo kubishania uhalisi wa dalili za kabla ya hedhi.

No comments:

Powered by Blogger.