Siri 20 usizozijua za kufurahia mapenzi

Matokeo ya picha ya wapenzi

NI Jumatatu nyingine tena imewadia marafiki zangu ambapo tunakutana katika uwanja wetu ule ule wa kupeana darasa hili maridhawa. Ninaamini mtakuwa wazima wa siha njema na mpo tayari kupokea kile nilichowaandalia kwa wiki hii. Karibuni.
Ndugu zangu, kuna mambo mengi sana yanazunguka, ambayo yanatakiwa kufanywa ili mtu aweze kufurahia mapenzi na mwenzake. Wakati mwingine kuna vitu ambavyo tunavikosea bila kufahamu, matokeo yake vinaleta matatizo kwenye ndoa hapo baadaye.

Leo nataka kukupa siri muhimu ishirini ambazo kwa hakika kama ukizizingatia, kwako mapenzi yatakuwa burudani ya aina yake. Huwezi kulia asilani katika maisha yako kwa sababu utakuwa umeshajua cha kufanya.

Ukweli ni kwamba, baadhi ya matatizo ambayo yanakuwepo kwenye ndoa, husababishwa na mwanzo mbaya wa wahusika, wakati walipokutana na kuamua kuanzisha uhusiano.

Wengi hawafikirii kuhusu hili, lakini ndiyo ukweli wenyewe. Hata kama upo kwenye ndoa, usiwe na shaka, mada hii ni kwa ajili yako, kwani zipo siri ambazo unaweza kuzitumia hata ukiwa tayari upo kwenye ndoa yako.

Hapa katika All About Love, kinachofanyika ni kukupa siri kuanzia mwanzo wa uhusiano ambao inatambulika kama urafiki, uchumba na baadaye ndoa. Kwa maneno mengine, kila aliye kwenye uhusiano, mada hii inamhusu.

Ikiwa upo ndani ya ndoa na mwanandoa mwenzako anaonekana hashibi chakula cha usiku au anavimbiwa, ndani ya siri hizi ishirini utapata tiba. Mathalani mwenzako hakuridhishi mnapokuwa faragha, mada hii ni kwa ajili yako. Yapo mengi ya kujifunza, wapo ambao wanatoa harufu mbaya sehemu za siri, wana maumbile madogo au wanashindwa kufanya kazi inavyotakiwa na hivyo kudharauliwa, nao nitazungumza nao.

Niseme tu, ni siri ishirini ambazo zipo sirini, lakini hapa tutazungumza kwa lugha ya kirafiki zaidi bila kuchafua hali ya hewa na mambo yataenda sawasawa. Haya sasa marafiki, twende tukaanze kuhesabu siri moja baada ya nyingine. Kama nilivyosema awali, kwamba nitaanza mwanzoni kabisa mwa uhusiano (urafiki), uchumba na baadaye ndani ya ndoa, ambapo huko ndipo kwenye kasheshe zaidi, maana hakuna ‘option' zaidi ya kukabiliana na tatizo.
Wengi tunafahamu kwamba, walio kwenye urafiki hata uchumba, wanaweza kuamua lolote kama wataona wenzi wao wana matatizo fulani. Ni rahisi kubadilisha uamuzi hata kama watakuwa wamefikia katika hatua ya mwisho kabisa.
All About Love haitarajii uingie kwenye matatizo hayo; lengo lake ni kukuandalia ndoa imara, bora itakayokuwa faraja ya maisha yako na siyo kilio. Anza kutiririka na siri hizo...

1. FANYA UCHAGUZI SAHIHI

Hapa ndipo watu wanapotakiwa kutumia akili zao mpaka zile za akiba, ukikosea hapa ni rahisi sana kuvurunda hapo baadaye. Uhusiano wenye nguvu, hujengwa na penzi la kweli. Acha kukurupuka, lazima ujihakikishie kwamba uliyenaye ni chaguo kutoka ndani ya moyo wako.
Najua una maswali; kwamba utawezaje kumjua mwenye mapenzi ya kweli, hiyo ni mada ambayo nimeshaandika mara kadhaa katika ukurasa huu na gazeti damu na hili,

Ijumaa. Kimsingi, kwa kufuata maelekezo hayo, mwenzi ambaye unatarajia kuwa naye katika maisha ya ndoa hapo baadaye, lazima msingi uwe ni uchaguzi sahihi.
Sikia, watu wengi waliokuwa na fedha, wamefilisika baada ya kuoa/kuoleawa na wenzi ambao si sahihi. Aidha, wapo wenye mafanikio makubwa sana, ambayo

wameyapata baada ya kuoa/kuolewa na wenzi sahihi. Rafiki zangu, si jambo rahisi kumpata yule aliye sahihi. Inahitaji utulivu.
Yapo mengi sana ambayo unapaswa kuyaangalia, ambayo nimekwishaeleza sana katika makala zangu zilizopita. Wakati nahitimisha kipengele hiki, shika neno moja tu; unapomchagua mwenzi wa maisha yako, hakikisha ni yule aliye sahihi! Tuendelee na kipengele kingine.
2. JIELEZE
Migogoro mingi baina ya walio kwenye uhusiano husababishwa na wenzi kutowafahamu vyema wenzao. Usiingie katika mkumbo huu, ni suala la kujieleza tu. Kumweleza mpenzi wako ulivyo, kutamfanya ajue vitu unavyopenda na usivyopenda. Aidha, kama unao udhaifu wowote wa kiafya na kadhalika, mweleze mwenzako.
Kumweleza kutamfanya ajiamini kuwa anapendwa. Kunaonesha unavyojiamini na unayetaka mwenzako ashirikiane na wewe katika hali uliyonayo. Si vibaya mwenzio

kukufahamu kwamba una hasira sana. Yes! Maana akishajua hilo, ataacha utani unaokaribia kukuudhi maana anajua vizuri kuwa una hasira za karibu.
Ipo mifano mingi sana, lakini kikubwa cha kushika katika kipengele hiki ni kuwa mkweli kwa mwenzako kuhusu maisha yako. Acha kumdanganya kwamba familia yenu
ina uwezo mkubwa, wakati ni wa kawaida. Kuwa mkweli, mapenzi si utajiri, ni hazina iliyojificha ndani ya moyo.

Kama anakupenda, anakupenda tu! Siku akigundua kwamba unamdanganya, pendo lake litapungua kwa kiasi kikubwa sana. Jieleze kwa uwazi na ukweli kutoka ndani ya moyo wako. Naye atakuheshimu na utakuwa umetengeneza mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye ndoa isiyo na migogoro.
Rafiki zangu, nilisema zipo siri ishirini, tumeshaona mbili, wiki ijayo tutaendelea na siri nyingine. Ni mada ndefu kidogo, lakini yenye elimu pana, itakayobadilisha kabisa mtazamo wako katika mapenzi. Tafadhali usikose! baadae....
AFYA yangu ni kielelezo tosha kuwa nimewaandalia kitu kizuri sana kwa ajili ya kupanua mawazo yetu juu ya mambo ya uhusiano na mepenzi.Nazungumzia siri ishirini ambazo kama zikitumika vyema, huongeza ladha katika mapenzi, lakini pia mateso na matatizo yatakuwa hayana nafasi kabisa kwa watu wa aina hiyo.
Nilianza wiki iliyopita, lakini kwa uchache sana nilieleza siri mbili za awali, leo tunaendelea na siri nyingine. Rafiki zangu, nawahakikishia kwamba, mara baada ya kumaliza kusoma mada hii, kila kitu kitabadilika.
Mtazamo wako juu ya mapenzi utakuwa mwingine kabisa, huwezi kubabaishwa kamwe. Bila kupoteza muda, rafiki zangu, hebu twende tukaone siri zinazofuata.

3. MPE UHURU
Wengi wanaamini kumbana mpenzi ni njia sahihi ya kumfanya awe mwaminifu, si kweli. Kuna wenye tabia ya kuvizia simu za wenzao na kuzipekua, si utaratibu mzuri. Mpe uhuru, usimbane! Kuonesha kumwamini sana mpenzi wako, kunamfanya naye aishi ndani ya uaminifu.
Kumchunga hakumnyimi kuendelea na mambo yake, sana sana atafanya kwa siri kubwa. Kumpa uhuru, kutamwogopesha, atajua yupo na mwaminifu ndiyo maana hafuatiliwi, hapo utakuwa umechochea naye awe mwaminifu kama wewe.

4. ACHA PAPARA
Katika hatua za mwanzo kabisa za uhusiano wenu, hutakiwi kuwa na papara katika jambo lolote. Kila kitu kifanywe kwa utaratibu. Huna sababu ya kurukia mambo, hasa makubwa.

Wengi wamekuwa na haraka sana ya kukutana kimwili, haya ni makosa makubwa sana. Haraka ya nini kama unatarajia awe wako wa maisha. Ngoja nikuambie rafiki yangu, unapoanza kuulizia mapema mambo ya faragha, unamfanya mwenzako ashindwe kukuamini.

Kwanza, atahisi wewe upo kwa ajili ya kutaka kujistarehesha tu, lakini pia anaweza kufikiria kwamba unapenda sana mambo ya chumbani. Kumfanya agundue kasoro hiyo ni tatizo kubwa sana kwako.

Hata hapo baadaye mtakapoingia kwenye ndoa, ni rahisi zaidi kukumbuka mambo ya zamani, kwamba yupo na mtu anayependa sana mambo ya mahaba. Kwa maneno mengine, hata akihisi tu au kusikia kwamba una mtu mwingine pembeni, atapeleka moja kwa moja hisia zake kwenye kuamini moja kwa moja juu ya jambo hilo.

Papara si jambo jema kabisa kwa mwenzi ambaye unatarajia awe wako wa maisha. Tulia, mchunguze kwanza. Kumbuka unatakiwa kufikiria kuhusu mustakabali wa maisha yako ya baadaye, kama ndivyo, huna haja ya kuharakisha mambo ya mapenzi.

5. JENGA URAFIKI
Ukitaka kutengeneza uhusiano wenye nguvu, basi zingatia zaidi urafiki. Kumfanya mwezi wako rafiki ni silaha kubwa na yenye nguvu katika kuuimarisha uhusiano.

Mwenzi wako anapojiona kama rafiki, anakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumza chochote, ikiwemo matatizo na migongano mbalimbali kama rafiki zaidi.


Hawezi kukuficha siri zake. Atakuwa na wewe muda wote na atakusogeza karibu yake kwa kila kitu. Hata penzi lenu pia litakuwa na nguvu zaidi. Urafiki ni kila kitu ndugu zangu.

Acha tabia ya kumkaripia mpenzi wako, jenga mazoea ya kujadiliana zaidi kuliko kutumia kauli za ukali. Rafiki zangu, yote hayo niliyoyazungumza yanajengwa na jambo moja tu; urafiki!

6. MSIFIE
Wengine wanaweza kushangazwa na kauli hiyo, lakini nataka kuwaambia kuwa kati ya mambo muhimu kabisa kumfanyia mpenzi wako na kulifanya penzi kuwa jipya ni kumsifia. Unapomwambia mwenzako kauli nzuri za kumbembeleza kuwa yeye ni mzuri, anakuvutia kwa kila hali, unajenga penzi.
Unamfanya anajihisi wa thamani, atajiamini kuwa yeye ni mkamilifu, si kwa watu wanaomzunguka pekee, bali hata wewe ambaye umemchagua na kumfanya awe wako.
Kama huna utamaduni wa kumsifia mpenzi wako, huu ni wakati wako wa kufanya hivyo kwa lengo la kuzidisha mapenzi na kuyapa nguvu.

7. SAIDIA KUKUZA UHUSIANO WENU
Kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha penzi linazidi kukua siku hadi siku. Kwa maana hiyo, wewe kwa nafasi yako unatakiwa kuhakikisha unakuwa mstari wa mbele kukuza uhusiano wenu.

Kuna mambo mengi sana ambayo yakifanyika, yanakuza uhusiano. Vipo vitu vya kufanya, kutoka pamoja ni njia mojawapo ya kukuza uhusiano. Rafiki zangu, mnapokwenda katika matembezi, husaidia kubadilisha mapenzi na kuonekana mapya.

Si lazima kwenda nje ya mji, kikubwa ni kuzingatia mfuko wako. Hata mkienda mahali pa kawaida tu, mkanywa juice na keki, bado ni nafasi nzuri kwenu ya kukuza uhusiano huo.

Kila mmoja ana wajibu wa kufanya hivyo, lakini hutakiwi kumsubiri mwenzako afanye, wewe kwa nafasi yako unatakiwa kuhakikisha unamfanya mwenzi wako afurahie uhusiano wenu. Kufanya hivyo, kutampa deni na yeye la kufanya hivyo kwako.
Bado kuna siri nyingi zimesalia, wiki ijayo tutaendelea. Tukimaliza kumi za kwanza, tutaingia kwenye siri nyingine kumi za mwisho ambazo zitakuwa zinahusu mambo ya ndani zaidi ya ndoa. 

8. MFANYE NAMBA MOJA
Kuna baadhi ya marafiki wana fikra potofu (hasa wanaume). Hawa wanaamini kumpa mwanamke nafasi katika maisha ni kumfanya akukalie. Si kweli. Mwanamke unapompa nafasi ya kwanza, anaufurahia uhusiano wenu.
Anajiona mwenye hadhi kubwa zaidi kwako, hutafuta njia za kukufanya umpende maradufu, kuliko kumuacha akijiona hana nafasi.

Ongozana na mpenzi wako kwenye kumbi za burudani, mialiko ya sherehe mbalimbali, lakini pia mpe kipaumbele kwa kila kitu. Hili halihitaji elimu ya darasani. Chunguza wenzako wanaowapa wenzi wao kipaumbele wanavyoishi.

Achana na mifumo ya kizamani, ukimpa mwenzako usawa anajiona ana nafasi kwako na thamani katika uhusiano mlionao.

9. MPE NAFASI
Hapa hakuna kitu kikubwa sana, ni kiasi cha kumpa nafasi katika mambo yako muhimu. Mathalan unataka kununua kiwanja Gongo la Mboto; Hata kama umeshaweka kila kitu sawa, lakini kumshirikisha tu, kutamfanya ajione mwenye nafasi kubwa kwako.

Hili si kwa wanaume pekee, hata wanawake nao wanapaswa kutoa vipaumbele kwa wanaume zao. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuongeza ladha ya mapenzi kwa wapendanao.


Inawezekana elimu hii imekupitia kushoto, hebu jaribu uone mafanikio yake.

Kumpa nafasi mwenzako katika mambo yako, tafsiri yake ni kumuamini na kumfanya azidi kujiamini kwako. Ni rahisi sana, lakini habari njema kwako ni kwamba, atakusikiliza kwa kila kitu, maana anajiona yeye ni sehemu yako kikamilifu.

10. MTAMBULISHE
Mapenzi ya siri yana ukomo wake marafiki zangu. Ngoja niwaambie, unapokuwa unapenda mapenzi ya siri sana, unampa wakati mgumu mwenzako.
Ni rahisi kufikiria kwamba, unafanya hivyo kwa kuwa ama hujiamini au una mtu mwingine. Weka mambo hadharani. Mtambulishe mwenzi wako kwa marafiki zako.

Jiamini, unapokutana na mtu uliyesoma naye zamani au kuishi naye sehemu moja, mwambie kwamba uliyenaye ni mwenzako na unatarajia kuingia naye kwenye ndoa.

Kufichaficha kunaondoa utamu wa mapenzi. Kunazidisha maswali ambayo hayana majibu. Kama yapo ni huyo mwenzako kujijibu mwenyewe. Kwa kawaida, hatajipa majibu mazuri.

Yatakuwa ya kinyume – yenye tafsiri mbaya. Kwamba yawezekana hutaki kumtambulisha kwa kuwa una mtu mwingine. Je, ni kweli? Kama ndivyo huna sababu ya kumpotezea muda mwenzako. Kama si kweli, basi amka. Gundua kwamba ulikuwa unafanya makosa na uanze ukurasa mpya.


11. GUSIA MAMBO YA KIIMANI
Kuzungumzia mambo ya dini kulingana na imani yenu, kutamsogeza mwenzako kwenye ukweli kuwa una lengo naye la kuungana katika maisha ya ndoa. Angalizo kwako ni kwamba, wakati unamweleza hayo, iwe kweli yanatoka ndani ya moyo wako.

12. WAHUSISHE VIONGOZI WA DINI
Ikiwa uhusiano wenu umekomaa, unatakiwa kuwashirikisha viongozi wa dini. Angalia mazingira, unaweza kwenda naye, au kwenda mwenyewe na kuwaeleza nia yako. Waambie wakuombee au wawaombee ili uhusiano wenu uwe na nguvu.

Kumbuka ndoa ni tendo la heri, hivyo shetani naye hutumia nafasi hiyo kuwaharibia! Kumuingiza Mungu katika uhusiano wenu kuna maana, mtakuwa katika ulinzi wenye nguvu zaidi.

Yamkini pia, kama uliyenaye si chaguo kutoka kwa Muumba atamuengua mikononi mwako na kukupeleka palipo sahihi. Usiogope, nenda kaonane na viongozi wa dini na uwaeleze kinagaubaga.

13. KAMILISHA TARATIBU ZA KIFAMILIA/KIMILA
Ikiwa una uhakika kuwa mwenzako ndiye uliyemkusudia (zaidi kwa wanaume) wajulishe wazazi wako, kisha anza taratibu za kimila na kifamilia. Tuma wazee wapeleke posa, lipa mahari, halafu sasa anza kutimiza maagizo mengine yote utakayoagizwa.

Ni njia ya kuelekea kwenye ndoa. Uhusiano wenye baraka za wazazi, si tu kwamba unakuwa na nguvu, bali una radhi za wazazi wenu wa pande zote mbili. Je, kwa hali hiyo uhusiano wenu hautaimarika? Bila shaka utazidi kuchanua.

Natamani sana kuendelea na vipengele vingine, lakini nafasi yangu hairuhusu, wiki ijayo tutaendelea,
0765203999

No comments:

Powered by Blogger.