SIMULIZI FUPI : MWANAMKE ALIUPONZA MGUU WANGU

maxresdefault.jpg

Nina mguu mmoja, mwingine niliupoteza katika ajali. Ningependa kusimulia ajali hiyo, ili kuwasaidia wenzangu ambao wanatenda yale yaliyonifikisha mimi hapa.
Nilikuwa mtumishi wa idara ya serikali mkoani Iringa kuanzia mwaka 1977 hadi 1983 nilipopata ajali ambayo ilibadili maisha yangu, kutoka yenye matarajio hadi maisha yaliyosheheni giza totoro.
Nikiwa hapo Iringa, familia yangu ilizoeana na familia nyingine ya bwana mmoja ambaye alikuwa na maduka ya vyakula. Mke wa bwana huyo alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi. Mke wangu alikuwa ni mwalimu wa shule ambapo mwanamke huyu alikuwa akifundisha.

Katika urafiki huo wa kifamilia, mimi niliingiwa ma ibilisi wa kumtamani yule mke wa mfanyabiashara, ambaye naweza kusema, alikuwa ni rafiki yangu, kwani kuzoeana kwetu kulikuwa kumepevuka kidogo. Mwanamke huyu naye kumbe alikuwa amevutiwa nami. Wakati huo nilikuwa bado kijana, ninayependeza.
Tulianza uhusiano mwaka 1979, miaka miwili baada ya mimi kufika Iringa na kujuana na familia hii. Wakati huo ndoa yangu ilikuwa na miaka sita tu, maana nilikuwa nimeoa mwaka 1973. Tulianza kukutana kwa siri na mwanamke huyu, ambaye alikuwa mdogo ukilinganisha na mumewe, kwani mumewe alikuwa ni mtu mzima kidogo wa miaka kama 50 na yeye mwanamke alikuwa na umri wa miaka kama 25.
Uhusiano wetu na mke wa jamaa yangu ambaye hapa nitamwita Mfanyabiashara, ulianza kwa kasi kubwa sana. Tulikuwa tumehemkwa kwa nguvu kubwa kiasi kwamba nilianza kuhofia. Nilijitahidi sana kuweka mipaka ili tusifikie mahali tukajisahau.
Mwaka 1981, habari zilianza kuvuja kuhusu uhusiano wetu. Mke wangu ambaye alikuwa anafundisha na huyu hawara yangu shule moja, huku wakiitana marafiki, aliniambia kwamba, kuna jambo linanong’onwa kwamba, nina uhusiano na huyo rafiki yake, mke wa mfanyabiashara, ambaye hapa mke huyo, nitamwita Waridi, ikiwa ni tafsiri ya Kiswahili ya jina lake halisi.
Niliposikia habari hiyo kutoka kwa mke wangu nilishtuka sana. Lakini nilimudu kujifaragua na kujitetea kiasi kwamba, ingekuwa ni mtu mwenye moyo mgumu sana, asingeweza kulainika.
“Watu hawapendi wakiona familia mbili zinaelewana, hasa familia kama zetu. Mimi bado kijana mdogo, nina kazi nzuri na fedha na wewe una kazi, hawa wenzetu wana biashara nyingi hapa mjini, ni lazima utasikia mengi. Shemeji Waridi hawezi hata kufikiria kuhusu upuuzi huo na mimi wala sijawahi hata kuota, siyo kwa Waridi, bali kwa mwanamke yeyote.” Nilimalizia kujitetea.
Nilimwonya sana Waridi baada ya kukutana. Aliniambia naye mume wake alikuwa amemuuliza kuhusu madai anayopata ya uhusiano wetu. Niliogopa sana. Lakini alisema, alikuwa amemudu kumtuliza kabisa na wala hilo halikuwa suala tena. Nilipata moyo na mapenzi yetu yakapamba moto zaidi.
Mwaka 1982, mke wangu alinisakama tena, safari hii akidai kwamba, ana vyanzo vya kuaminika kuhusu uhusiano wetu na Waridi. Nilimwambia kwamba, sina haja ya kubishana naye, ila niko tayari kushika kitabu cha dini tuape kwa laana zote.
Nilipomwambia hivyo alinywea. Nilimwambia hivyo makusudi, nikijua kwamba, alikuwa ni mtu wa dini sana. Aliogopa akiamini kwamba, kusema kwangu vile, kulikuwa na maana ya uhakika kwamba, sikuwa nashiriki jambo hilo.
Alisema, hao watu wanaomwambia, wana sababu gani ya kudanganya. “Nimekwambia watu wana hila mke wangu. Dini inasema, kufumania ni kuona kwa macho na siyo mtu mmoja, bali wanne. Unadhani inasema hivyo bure tu, hapana, ni kwa sababu ya mambo kama hayo.” Nilizidi kumfanya aniamini.
Ilibidi sasa tubadili mikakati yetu na Waridi. Nilikuwa nachukua gari la kazini na tukawa tunaondoka wote hadi nje kabisa ya mji wa Iringa. Wakati mwingine tulikuwa tunaingiza gari porini na kufanyia mambo yetu garini na hii ilitupa raha zaidi. Tuliamua kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba, kuingia gesti za pale mjini ilikuwa ni kujichongea bure.
Ilisaidia kwani mwaka 1982 uliisha bila kero na 1983 ukafika hadi Juni, bila kusikia lolote. Lakini kama inavyosemwa mkizini mtafumwa tu, hata iweje, ilitokea kwa aibu na fadhaa.
Hiyo Juni, 1983 mume wa Waridi alipata safari ya kwenda Malawi kibiashara. Wiki hiyo nami nilikuwa na safari ya kwenda Dar es salaam. Tulikubaliana na Waridi kwamba, tuondoke wote wakati mimi naenda Dar es salaam, tuje hadi Morogoro, tulale pale hadi kesho yake, mimi niendelee na safari naye arudi Iringa.
Kwa bahati nzuri shule zilikuwa zimefungwa. Waridi alisema angemwambia mumewe akirudi kwamba, alikuwa ameenda Morogoro kumwona dada yake ambaye alikuwa ameumwa ghafla. Niliona ni wazo zuri. Ni kweli, tuliondoka wote.
Tulifika Morogoro na kupiga kambi. Waridi alikwenda kwa dada yake na kumwambia kwamba, amesikia kwamba anaumwa, hivyo amekuja kumwona. Ni kweli, alikuwa anaumwa kidogo wiki hiyo, lakini alikuwa na nafuu. Baada ya kuzungumza naye kwa muda wa saa mbili alimwaga kwamba anarudi Iringa.
Alisindikizwa hadi stendi, ambapo mimi nilijitokeza na gari na kujifanya tunajuana na Waridi na kwamba natoka Dar es salaam na ninaenda Iringa. Waridi naye alijifanya ananiomba lifti ambapo nilimkubalia. Dada yake alisema, “una bahati kweli, haki ya Mungu.” Wenyewe tuliona tunafanya ujanja mkubwa sana.
Tuliondoka hadi mzunguko wa Msamvu na kurudi mjini. Tulilala Morogoro na asubuhi yake Waridi aligoma kurudi Iringa, akisema ni lazima afike na kulala Dar. Niliogopa kidogo, lakini nami wakati huu Ibilisi alikuwa amenikalia kichwani vibaya sana. Nilimkubalia. Tuliondoka Morogoro saa 1:45 asubuhi kuelekea Dar.
Ilikuwa ni kama kilomita mbili tu kutoka Mlandizi, ndipo ilipotokea ajali. Nilikuwa nimeshuka kimlima kutokea mji wa mlandizi na kupanda, halafu nikakanyaga mafuta hadi gari likawa linaenda kilomita 100 kwa saa. Nilisikia mlio mkubwa sana na gari iliyumba na nikanyang’anywa usukani. Halafu niliona tukipaishwa na kutupwa kando ya njia kwenye mti wa mwembe.
Upande aliokuwa amekaa Waridi, ukifikia kwenye shina la mwembe. Sikusikia tena kitu, wala kujua kilichotokea. Ni siku ya pili jioni niliposhtuka nikiwa Muhimbili. Nilimwona mke wangu akiwa kando ya kitanda changu pamoja na watumishi wa makao makuu ya idara niliyokuwa nafanyia kazi. Nilihisi kama wepesi fulani huko chini. Nilipokagua, niligundua kwamba, sikuwa na mguu wa kushoto.
Ilinichukua muda kabla sijakumbuka kilichotokea. Polepole nilikumbuka kutoka Iringa, Morogoro hadi Mlandizi. Sikukumbuka tena kitu. Ilinichukua muda kukumbuka ajali na kumkumbuka Waridi. Nisingeweza kumuuliza mke wangu au yeyote pale kuhusu Waridi, lakini nilikuwa na uhakika kwamba, alikuwa amekufa.
Nilianza kububujikwa na machozi. Nilijaribu kusema, lakini sikuweza, ni midomo tu iliyokuwa ikicheza.
“Amekufa, amekufa,uso wangu sasa naupeleka wapi, naupeleka wapi jamani…” Mke wangu alisema na kuangua kilio. Nilimwelewa. Wale watumishi wenzangu walimtuliza, “tuangalie na kujali hali ya mgonjwa kwanza,” walimwambia.
Ni kweli, Waridi alikufa palepale kwenye tukio la ajali na mimi ni bahati tu kupona na kukatwa mguu mmoja badala ya miguu miwili na mikono. Nilikuwa na uhakika kwamba, makovu ya mwilini baada ya kupona yangekuwa yanatisha.
Kila kitu kilifahamika baada ya siku tatu tu. Mume wa marehemu Waridi alirejea kutoka safari na kusimuliwa kila kitu. Aliahidi mbele za watu kwamba, angenimaliza na mimi, iwe kwa mvua au jua. Nilipopata taarifa hizo nilicheka kwa sababu, niliona akifanya hivyo angekuwa amenitua mzigo mzito. Labda aliambiwa baadaye nilivyokuwa nasema, ndiyo maana hakufanya lolote.
Baada ya miezi mitatu, nilitoka hospitalini nikiwa na mguu mmoja. Nilikuwa na nafuu kidogo. Mke wangu alishaanza uhusiano na yule mfanyabiashara na hakunificha. Ilibidi nifike mahali niombe talaka. Talaka ilitolewa na kuwaacha waendelee. Hatimaye mwaka 1985 walioana, ingawa ndoa yao ilivunjika mwaka 1990 kwa makeke na vurugu kubwa.
Mimi nilifukuzwa kazi mwaka 2003, na nikaendelea na shughuli zangu binafsi. Nilikuja kuoa mwaka 1987, mke ambaye tunaelewana sana na amekuwa ndiye kiongozi wangu kwa mambo mengi. Tuna watoto wanne.
Kuna watu wanapenda kuniita “Kaguu” kwa siri. Nawaomba waniite kabisa kwa nguvu, kwa sababu ninastahili.

MWISHO


No comments:

Powered by Blogger.