JALI HISIA ZAKE, ACHA KUANGALIA HURUMA YAKE KWAKO
SI kwamba atakupenda sababu ana huruma na hisani, hapana. Anapaswa kukupenda kwa sababu ya msukumo wa hisia za dhati juu yako. Huruma huwa na kikomo ila nafsi ya upendo haichoki kupenda.
Wapo wanaonyanyaswa na wapenzi wao. Wengine kila siku wanaambiwa hawatakiwi ila hawataki kuamini. Badala ya kuamua kufanya uamuzi wanaotakiwa kuufanya, wao hulia na kusema basi nionee huruma. Ni nani kakwambia watu wanapendana kwa sababu ya huruma?
Kama leo akikupenda kwa sababu ya huruma tambua katika moyo wake nafasi ya upendo itakuwa bado haijajaa na kwa sababu hiyo, siku yoyote atatafuta wa kujaza nafasi hiyo.
Huruma unayoihitaji ni lazima iamuliwe na upendo ndiyo iwe endelevu. Ila kama anakuwa na wewe kwa sababu unalia sana au kwa sababu umemuomba sana, jua upo katika kuti kavu. Muda wowote tegemea kuanguka.
Nimeona watu wengi wakilia katika uhusiano wao. Wapo wanaolia na kusema fulani ana roho mbaya sana. Ni kweli huenda iko hivyo. Ila jua suala la mapenzi ni la hisia. Mambo ya roho mbaya au nzuri yanapatikana kama ukiwa na mtu mwenye hisia kamili na wewe au mwenye hisia batili na wewe.
Walio katika uhusiano na machaguo ya mioyo yao, wana raha sana. Wanaoneana huruma kwa dhati na wana furaha timilifu. Ila kama upo kwa sababu ya huruma au kwa sababu umemuahidi kuwa utampa kila anachotaka jua upo katika penzi hatari. Penzi salama ni lile wahusika wanaunganika kwa msukumo kamili wa hisia zao. Lile lenye kuwafanya kila mmoja ajihisi amani na faraja kila anapomuona mwenzake.
Nimeshuhudia mahusiano mengi ya mtindo wa huruma au ahadi nyingi. Wengi wa wahusika katika mahusiano ya namna hii, huwa hawana amani timilifu na mahusiano yao huwa ya upande mmoja. Mmoja anampenda mwenzake huku mwingine akiwa katika uhusiano kwa sababu ya kusukuma siku tu. Haya ni kwa namna gani utayaita mahusiano ya kimapenzi?
Utalia sana, utateseka sana kama ukilazimisha kuwa na mtu asiye na hisia za dhati na wewe. Hata kama unampenda vipi, ila kama anasema hakutaki kwa dhati basi jua ni bora ukakubali yaishe. Kama ukilazimisha utakuwa mtumwa katika uhusiano husika huku ile furaha unayotegemea kuikuta usiikute. Ni kwa namna gani upate furaha katika mahusiano yasiyo kuhitaji?
Wanaopendana kwa dhati karibu kila muda hutaka kuwa pamoja. Na kila wanapokutana nafsi zao na miili yao inakuwa na njaa na kiu ya kila mmoja ila si katika mahusiano ya aina nyingine. Kama kuna mmoja kamsukuma mwenzake amkubalie bila mwenzake kuwa na uhitaji, basi jua kuna hatari katika uhusiano huo.
Kubali kulia leo. Kasema hakupendi? Usijali, achana naye. Inauma ila hakuna jinsi. Kama ukilazimisha, jua kesho utakuja kulia na kujuta zaidi ya leo. Mapenzi ni kitu rahisi sana. Ila pia mapenzi ni kitu kigumu sana. Kama ukilazimisha mapenzi ni kitu kigumu sana. Nimeona wengi wakilia na kulaani mapenzi kwa mtindo huu. Walikuwa hawatakiwi ila walitumia akili nyingi, wakatumia mali nyingi na kisha wakatumia maneno mengi na hatimaye wakakubaliwa. Matokeo yake?
Ni vilio na simanzi katika maisha yao. Ila pia wapo ambao badala ya kutafuta mapenzi ila mapenzi yaliwatafuta wao. Leo wako na furaha na amani katika maisha yao. Wanakula wanachojisikia na kufurahia kila hatua ya mahusiano yao. Kuwa makini.
No comments: